Wadau wahofia Sheria ya Takwimu

11Sep 2018
Na Waandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Wadau wahofia Sheria ya Takwimu

WADAU kadhaa wameonyesha hofu marekebisho ya Sheria ya Takwimu iliyowasilishwa bungeni jana, wakisema kuwa sheria hiyo itakwaza shughuli za utafiti.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi.

Jana serikali iliwasilisha bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria ya Takwimu kifungu cha 37(4) kwa kuweka masharti kwa mtu yeyote atakayechapisha au kusambaza taarifa za kitakwimu kinyume cha sheria hiyo, atakuwa ametenda kosa la jinai.

Katika mabadiliko hayo, kuna masharti kuwa mtu yeyote aliyepata kibali cha kutumia takwimu rasmi za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), hatachapisha au kutoa taarifa husika kwa umma bila kupata kibali cha ofisi hiyo.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, alisoma marekebisho ya sheria hiyo jana bungeni wakati akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba tatu wa mwaka 2018.

"Kifungu kipya cha 18 na 19 kinapendekeza kuwa Mtakwimu Mkuu atakuwa na mamlaka ya kuanzisha, kurekebisha au kufuta takwimu rasmi zilizokusanywa kwa njia ya utafiti au sensa."

"Na kwamba mtu, taasisi ya serikali au wakala hataruhusiwa ukusanyaji wa takwimu rasmi pasipo kupata kibali cha Mtakwimu Mkuu, lengo la marekebisho haya ni kumwezesha kusimamia ipasavyo ukusanyaji wa takwimu rasmi," alisema Dk. Kilangi.

Dk. Kilangi alisema kifungu cha 17(3) (a) na (b) cha sheria hiyo kinaeleza kuwa NBS katika kutekeleza jukumu la utaratibu wa takwimu, itatoa kanuni za utendaji ambazo zitazingatiwa na wakala zinazotoa takwimu rasmi.

Alisema pia NBS itaandaa benki ya takwimu za taifa kwa kutumia benki ya takwimu iliyoanzishwa na wakala husika.

"Muswada katika sehemu hii unapendekeza kifungu hicho kirekebishwe kwa kuweka masharti yatakayowezesha kanuni za utendaji kazi kuzingatiwa pia na taasisi zingine za serikali, na NBS kutumia benki ya takwimu ya taasisi ya serikali," alisema Dk. Kilangi.

MAONI YA UPINZANI

Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Wizara ya Katiba na Sheria, Ally Salehe, alisema marekebisho hayo yamejikita kudhibiti utafiti utakaokuwa unafanyika na kuwaeleza wananchi matokeo ya utafiti huo.

Alisema mapendekezo hayo yanapoteza dhana ya kufanya utafiti na matokeo yake kuwafikia wananchi husika wa utafiti huo.

Kuhusu mtafiti kuwasiliana na NBS kabla hajawasilisha utafiti wake, Salehe alisema: "Katika hili la mashauriano Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuna uwezekano mkubwa kuwa ikawa ni kumwambia mtafiti kurekebisha matokeo ya utafiti uendane na matakwa ya NBS au kufutwa kwa utafiti husika."

Salehe ambaye pia ni Mbunge wa Malindi, alisema lengo la utafiti ni kutafuta suluhisho la tatizo na siyo kushindana na serikali.

Akiwasilisha maoni na ushauri wa Kamati kuhusu Muswada huo, sehemu ya Mtakwimu Mkuu kupewa mamlaka ya kusimamia na kudhibiti usambaji wa takwimu nchini, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, alisema pendekezo hilo litaimarisha usimamizi, udhibiti wa upatikanaji wa matumizi ya takwimu nchini kwa mujibu wa sheria.

"Hatua hii itaiwezesha serikali kupata takwimu nyingi zaidi ambazo itazitumia katika kupanga mipango ya maendeleo ya sekta mbalimbali nchini na kustawisha jamii," alisema Mchegerwa.

HOFU YA WADAU

 

Wadau mbalimbali wameomba kwamba kabla ya kupitishwa kwake wasubiri wapate maoni ya kutosha kutoka kwa wadau wa takwimu, ili kuhakikisha wanaboresha na kuja na sheria bora itakayokidhi matakwa ya wananchi.

Dk. Benson Bana, Mwenyekiti mwenza wa Taasisi ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia (Redet), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema ili kupata sheria nzuri na bora lazima maoni ya wadau hao muhimu yashirikishwe kwanza na kupewa kipaumbele.

Alisema anaamini kwamba endapo muswada huo utapelekwa kama ulivyo na sheria ikapitishwa, utawanyima wananchi fursa ya kupata taarifa.

“Sheria hii imezungumzwa sana, lakini kwa namna muswada ulivyo, endapo itapita kama ilivyo itaongeza urasimu mkubwa wa kupata taarifa, ni vema hata kama wanasema kibali kitoke kwa Mtakwimu Mkuu waainishe ni utafiti upi siyo kila utafiti," aliasema Dk. Bana na kuongeza:

“Nasema hivyo kwa sababu zipo taasisi ambazo zinaaminika kwa kufanya utafiti bora na zimekuwa zikitumiwa sana, mfano Benki ya Dunia, utafiti wake ni nzuri na unatumika sana, kwa hiyo sheria kama hizi ni lazima wadau washirikishwe ipasavyo na ndiyo njia nzuri ya kupunguza malalamiko."

Naye aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Kijo Bisimba, alisema marekebisho hayo si ya kusaidia wananchi katika kupata taarifa sahihi, bali yataathiri upatikanaji wa taarifa sahihi katika mambo mbalimbali muhimu.

“Sisi tumeuona muswada huo, lakini kama wanataka kutenda haki, tunaomba wasiupitishe watoe nafasi pia kwa wadau kwa sababu mbali na kuathiri wananchi, lakini hata katika vyuo vyetu vikuu wataathirika," alisema Dk. Bisimba.

Imeandikwa na Gwamaka Alipipi (Dodoma) na  Elizabeth Zaya (Dar).