Yanga yamtetea Aziz Ki

27Apr 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga yamtetea Aziz Ki

KLABU ya Yanga imesema kuwa mchezaji wake raia wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki, ana mchango mkubwa licha ya kudaiwa hana msimu mzuri na amekuwa na kiwango cha kupanda na kushuka.

 

Afisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema jana kuwa kwenye kikosi cha Yanga, hakuna kiungo mwenye mabao manane na 'assist' nne zaidi ya Aziz Ki, huku akisema kupanda na kushuka kwa mchezaji ni jambo la kawaida.

"Kupanda na kushuka kunamtokea mchezaji yoyote duniani, kama inaweza kumtokea hata Cristiano Ronaldo au Lionel Messi, basi inaweza kumtokea mwingine yoyote. Tunavyojua Aziz Ki ni mchezaji ambaye anaweza kukupa matokeo chanya, au matokeo yasiyotarajiwa muda wowote ule kwenye mechi yoyote.

"Sitaki kuangalia sijui hajazoea mazingira au msimu wake wa kwanza, lakini alichokifanya tuna kila sababu ya kumpigia makofi kwa sababu amefikisha mabao manane na 'assist' nne, maana yake ameshachangia mabao 12 kwenye Ligi Kuu, achilia mbali mechi za kimataifa. Kwa hiyo licha ya kupanda kwake na kushuka, pamoja na kwamba mnasema hana msimu mzuri, lakini kwenye kikosi chetu hakuna kiungo mwenye namba nzuri kama zake," alisema Kamwe.

Alikumbusha kuwa kiungo huyo aliyesajiliwa msimu huu akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, ndiye anayeisababisha Yanga kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika kwa sasa kwa bao lake la ugenini alilolifungwa dhidi ya Club Africain ya Tunisia.

"Ni kiungo aliyeipeleka Yanga hatua ya makundi, sijui nyie mnamuangalia vipi, lakini sisi tunajua kuwa ni mmoja kati ya wachezaji wetu bora kabisa msimu huu huwezi kuacha kumtaja Aziz Ki," alisema.

Kumekuwa na maneno kwa wadau wa soka kuwa bado mchezaji huyo mpaka sasa hajaonyesha kiwango kile alichokuwa akionyesha alipokuwa klabu yake ya ASEC Mimosas kilichokuwa kikionekana msimu uliopita kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, timu yake ikiwa kundi moja na Simba.

Baadhi yao wanasema kiwango chake kimekuwa ni cha kupanda na kushuka, akifanya vema baadhi ya mechi na nyingine akipotea.

Mchezaji hiyo alisajiliwa mwanzoni mwa msimu huu kwa usajili uliotia fora, na kuwa gumzo kubwa nchini