Amesema wanadakika 90 zingine zilizosalia ambazo ni muhimu kwao kuzitumia vizuri nyumbani na wachezaji wanatakiwa kusahau matokeo yaliyopita na kuangalia mechi ijayo.
Yanga inatarajia kushuka dimbani Jumapili hii wakiwa wenyeji wakiwakaribisha River United katika dimba la Benjamin Mkapa Dar es Salaam, baada ya kufanikiwa kurejea na ushindi wa mabao 2-0 kutoka nchini Nigeria.
Akizungumza na Nipashe jana, Nabi alisema kushinda ugenini haina sababu ya wako kuwa tayari wamefanikiwa kwa asilimia kubwa kufuzu nusu fainali kwa sababu bado wana kibarua cha dakika 90 za kipindi cha pili.
Alisema kila mchezaji anatambua namna walivyopoteza dhidi ya timu hiyo mwaka 2021 na sababu wanazitambua na wamezifanyia kazi, wachezaji hawatakiwi kuridhika na matokeo waliyoyapata Nigeria.
“Tunatambua wapinzani wetu Rivers United sio timu mbaya na rekodi ya kupoteza mbele yao mwaka 2021 tunakumbuka, mechi zote tutapambana kupata ushindi wa jumla ili kusonga mbele kwenye hatua hii ya kimataifa.
Kushinda mechi ya ugenini ni mafanikio, lakini hatujaridhika kuishia hapo lazima tupambane kushinda mechi ya nyumbani na lazima wachezaji waonyeshe juhudi ili kupata matokeo mazuri,” alisema Nabi.
Naye Kocha msaidizi, Cedric Kaze alisema nyota wao, Bernard Morrison ni majeruhi na hakuwepo katika mchezo uliopita dhidi ya Rivers United baada ya kuumia kwenye mazoezi.
Alisema Morrison alikuwa katika mipango ya mchezo uliopita na Rivers United, lakini hakufanikiwa kucheza baada ya kupata shida ya misuli na mazoezini.
“Hatukuweza kulazimisha kucheza mechi iliyopita na kumuacha apone na tunatarajia kuwepo kwenye mipango ya mechi ijayo kwa sababu ni mchezaji muhimu na anaweza kufika katika eneo la hatari na kutengeneza madhara kwa wapinzani na kupata matokeo chanya,” alisema Kaze.
Alisema watamtumia kwenye mchezo wa marudiano kwani ni mchezaji mwenye uzoefu wa kutosha kwani ameshacheza michezo kama hiyo.
Aidha Kaze alisema licha ya mwanzo mzuri ugenini bado wana dakika 90 kwenye uwanja wa Mkapa katika mchezo wao wa marudiano.
"Ninaomba wachezaji wasibweteke na ushindi tulioupata ugenini wafahamu bado tuna dakika 90 ambazo zinatusubiri kwenye uwanja wetu wa nyumbani,” alisema.
Kocha huyo alisema wataandika historia endapo watamaliza hizo dakika kwa ushindi na kuomba mashabiki wajitokeze kwa wingi siku ya mchezo kwa lengo la kuwapa nguvu wachezaji.
"Tutaandika historia ya kuitoa Rivers United kama tutafanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika,”.
Kikosi cha Yanga kimerejea nchini jana na kuingia kambini moja kwa moja kwa ajili ya mchezo huo wa Jumapili kwa ajili ya kutafuta ushindi ambao utawapeleka katika hatua ya nusu fainali.










