-wote wakiwa kileleni katika mbio za kiatu cha ufungaji bora.
Yanga kama imelipa kisasi na nyongeza juu kwani katika mechi ya mzunguko wa kwanza Oktoba 4, mwaka jana, ilikubali kipigo cha mabao 2-1 kwenye mechi iliyopigwa Uwanja wa Highland Estates, Mbrali mkoani Mbeya.
Kiungo huyo raia wa Burkina Faso alitoa pasi tatu za mabao jana, hivyo kufikisha 'assist' tano mpaka sasa kwenye Ligi Kuu.
Aidha, Kiungo mshambuliaji raia wa Jamhuri ya Kidemomkasi ya Congo, Maxi Mpia Nzengeli, naye alifunga bao moja akifikisha mabao tisa huku Mudathir Yahaya akiendeleza moto wake wa kufunga mfululizo, akipachika bao tena katika mechi ya jana na kufikisha mabao manane.
Pacome Zouzoua naye alifikisha mabao saba akifunga moja, huku Augustine Okrah akifunga bao la kwanza akiwa na timu hiyo msimu huu, baada ya kusajiliwa kipindi cha uhamisho wa dirisha dogo.
Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 49, ikiwa imepachika mabao 47 katika michezo 18 iliyocheza, ikiendelea kuyoyoma na kuziacha timu zingine, na kuonekana kuusogelea ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya tatu msimu huu.
Ihefu ndiyo waliouanza mchezo kwa kasi, na sekunde ya 40 tu walikuwa wameshapiga hodi kwenye lango la Yanga, kwa Joseph Mahundi kuambaa na mpira wingi ya kushoto, akapiga krosi ambayo ilikosa muunganishaji, ikaokolewa na mabeki wa Yanga.
Mpira uliookolewa ulimkuta Duke Abuya ambaye shuti lake liliwababatiza walinzi wa Yanga na kumrudia mkononi ikawa faulo.
Hilo ndilo shambulizi pekee la hatari kufanywa na Ihefu dakika zote za kipindi cha kwanza.
Yanga ilijibu dakika ya tatu wakati Yao Kouassi alipokimbia na mpira wingi ya kulia na kumimina krosi ambayo ilishindwa kutendewa haki na Pacome Zouzoua ambaye alipiga hewa.
Dakika sita baadaye, Pacome alirekebisha makosa yake alipoukwamisha mpira ndani ya wavu, akimalizia pasi ya juu kutoka kwa Aziz Ki, likiwa ni bao lake saba kwa kwenye Ligi Kuu msimu huu.
Kipa wa Ihefu, Khomein Aboukakar, alifanya kazi ya ziada ya kuruka juu na kuuwahi mpira wa krosi ya Nicson Kibabage, kabla mpira haujamfikia Mudathir dakika 18 ya mchezo, huku mchezaji huyo akikosa bao la wazi dakika ya 25, alipopaisha mpira akiwa ndani ya eneo la hatari, akiunganisha krosi ya Yao.
Mudathir alirekebisha makosa yake dakika ya 29, alipofunga bao la pili, akimalizia pasi mpenyezo ya Aziz Ki.
Kipindi cha pili, Ihefu ilionekana kupoteana hasa kwenye safu ya ulinzi, ambapo iliwapa nafasi Yanga kutawala na kuweza kupachika mabao matatu mengine.
Aziz Ki alifunga bao la tatu dakika ya 67 akiwa amezungukwa na mabeki wa Ihefu, ambapo baada ya kupata pasi kutoka kwa Pacome, alizunguka na kuachia shuti dhaifu, lililojaa wavuni.
Winga raia wa Ghana, Okrah aliyeingia kipindi cha pili, aliipatia Yanga bao la nne dakika saba kabla ya mechi kumalizika, alipotanguliziwa mpira mrefu na Aziz Ki, akawatoka na kuwazidi mbio mabeki wa Ihefu kabla ya kuuweka wavuni.
Dakika mbili baadaye, Nzengeli ambaye naye aliyeingia kipindi cha pili, alifunga kitabu cha mabao kwa Yanga, alipoachia shuti kali lililogonga mwamba wa juu na kudunda chini, waamuzi wa mchezo wakaamuru ni bao, ingawa picha za marejeo zilizonyesha mpira ulidunda nje ya mstari wa lango.
Kipindi hicho cha pili kwa nyakati tofauti, Ihefu ilifanya majaribio kadhaa langoni mwa Yanga, lakini wachezaji wao walionekana kutetemeka linapokuja suala la kuuweka mpira ndani ya wavu.
Elivis Rupia ndiye aliyekosa mabao mengi ya wazi, akifuatiwa na Rafael Daudi ambao kama wangetulia wangeweza kufunga mabao katika mchezo huo.
Kipigo hicho kinaifanya Ihefu kushuka kutoka nafasi ya nane hadi ya 10 ya msimamo ikibakia na pointi 23, mabao 18, ikiwa imeshacheza mechi 20 mpaka sasa.