Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga watakutana na vigogo hao kutoka Afrika Kusini mechi ya kwanza wakianzia nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kati ya Machi 29 na 31, mwaka huu.
Kumbukumbu zinaonyesha mara ya mwisho timu hizo zilikutana mwaka 2001 katika hatua ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mechi ya kwanza ilichezwa Afrika Kusini na kumalizika kwa wenyeji kuondoka na ushindi wa mabao 3-2.
Katika mchezo wa marudiano uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Yanga walilazimishwa sare ya mabao 3-3 na hivyo kuondolewa katika michuano hiyo kwa jumla ya mabao 6-5.
Akizungumza na Nipashe, Rais wa Yanga, Hersi Said, amesema katika mpira hakuna kinachoshindikana, hivyo uongozi na benchi la ufundi wanajipanga vyema kuhakikisha wanaepuka yaliyowakuta miaka 23 iliyopita.
Hersi amesema Yanga haina hofu yoyote ya kukutana na mpinzani huyo kwa sababu wana wachezaji wenye viwango vizuri na benchi la ufundi imara na kwa sasa kazi yao ni kujiandaa vyema kuwakabili Wasauzi hao.
"Tunafahamu wapinzani wetu wana timu nzuri, timu inayofanya vizuri Afrika, lakini huwezi kubeza pia ubora wa kikosi chetu, tumepokea droo iliyotolewa na tunaanza maandalizi yetu, benchi la ufundi litafanya kazi yake na uongozi utajipanga kuhakikisha tunafanya vizuri," Hersi amesema.
Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema hakuna kinachoshindikana katika soka na yeye binafsi anaifahamu vyema Mamelodi Soundowns.
Gamondi amesema timu zote nane zilizofika hatua hiyo ni bora, hivyo hakuna mechi itakayokuwa nyepesi.
"Tutaandaa mbinu za kukabiliana nao, mchezo wa nyumbani ni mchezo muhimu zaidi kwetu, naifahamu Mamelodi vizuri, tupo tayari kukabiliana na tuna muda wa kujiandaa," amesema Gamondi.
Endapo Yanga itafanikiwa kusonga mbele katika michuano hiyo, hatua ya nusu fainali itacheza dhidi ya mshindi wa jumla wa mchezo kati ya Esperance de Tunis ya Tunisia au Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Timu nyingine ya Tanzania iliyofuzu kucheza hatua ya robo fainali ya mashindano hayo yanayoendeshwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ni Simba na yenyewe katika hatua hiyo itakutana na Al Ahly ya Misri, Wekundu wa Msimbazi pia wakipangwa kuanzia nyumbani.