Yanga yaiandalia Bamako dozi nene

06Mar 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga yaiandalia Bamako dozi nene

WAKATI kikosi cha Real Bamako kutoka Mali kikiwasili nchini alfajiri ya kuamkia jana, Klabu ya Yanga imesema imeandaa dozi kubwa zaidi kwa timu hiyo kuliko hata ile iliyotoa kwa TP Mazembe ambayo walishinda mabao 3-1 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Februari 19, mwaka huu.

 

Mkurugenzi wa Mashindano wa Klabu hiyo, Saad Kawemba, amesema maandalizi yote ya mechi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika yamekamilika na sasa wanachosubiri Jumatano ambapo mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, saa 1:00 usiku, ikiwa ni ya raundi ya nne ya Kundi D.

"Maandalizi yote ya mchezo huo yameshakamilika, mchezo ni Jumatano, wageni wetu wamewasili alfajiri ya leo (jana). Usiku wa Machi 8 kwa Mpaka, tunahitaji kuubadilisha kuwa wa furaha si kwa wanachama na mashabiki wa Yanga tu, bali kwa Watanzania wote. Tunataka tufanye zaidi ya vile tulivyofanya kwenye mechi dhidi ya TP Mazembe, tunachoomba ni watu kujitokeza kwa wingi," alisema Kawemba.

Yanga, iko nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo kwa pointi nne, na iwapo itashinda itafikisha pointi saba sawa na vinara US Monastir ya Tunisia ambao siku hiyo watakuwa jijini Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuivaa TP Mazembe inayoshika nafasi ya tatu kwa pointi zake tatu.

Baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, viongozi na wachezaji wa timu hiyo wamesema wameamua kuwasili nchini mapema kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa, pamoja na kupata muda zaidi wa maandalizi.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mchezaji Bourama Togola, alisema wamejiandaa kikamilifu, ingawa hawezi kusema moja kwa moja kama watashinda mechi hiyo.

"Tumejiandaa sana kwenye mechi hii, siwezi kusema tutashinda, tutatoa sare au tutafungwa, huu ni mpira, lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutashinda.

"Tumekuja mapema kwa sababu ya kuzoea hali ya hewa ya Tanzania, lakini pia kupata muda wa maandalizi ya mechi yenyewe kwa sababu umuhimu wa pointi tatu utatuongezea matumaini ya kusonga mbele kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hii," alisema mchezaji huyo ambaye angalau ana uwezo kidogo wa kuongea lugha ya Kingereza.

Jumapili iliyopita, Yanga ilifanikiwa kuidhibiti Real Bamako na kutoka sare bao 1-1, kwenye Uwanja wa 26 Mars nchini Mali.