Mbinu za kuweza kutimiza lengo hilo.
Kocha Mkuu wa Simba Robertinho Oliveira, amesema tayari ameandaa silaha zake vizuri huku akiwapa baadhi ya wachezaji majukumu maalum ya kuhakikisha wanapata pointi tatu katika mchezo huo baada ya ule wa awali ugenini kushinda 1-0.
Simba inahitaji kuvuna pointi tatu katika mchezo huo wa nyumbani ili kuweka matumaini yao sawa ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo, wakati huu wakiwa nafasi ya tatu na pointi zao tatu nyuma ya vinara Raja Casablanca ya Morocco yenye alama tisa na Horoya ya Guinea ambayo imeshavuna pointi nne huku Vipers ikiburuza mkia na pointi yake moja.
Wapinzani hao wa Simba wanatarajia kutua nchini leo, tayari kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa kesho, Jumanne katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam majira ya saa 1:00 usiku.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda, alisema kikubwa wanachohitaji ni safu yao ya ulinzi kuimarika na kujitahidi kutoruhusu washambuliaji wa Vipers kupata nafasi ya kutikisa nyavu.
Alisema jambo lingine ni safu ya ushambuliaji kuhakikisha wanatumia vema kila nafasi wanazotengeneza katika mchezo huo lengo lao likiwa ni kutafuta ushindi na idadi nono ya mabao.
Kuhusu mshambuliaji Moses Phiri ambaye alikuwa na kiwango kizuri katika michuano hiyo kabla ya kuumia, Mgunda aliwatoa hofu mashabiki akisema suala la kuanza katika mchezo huo lipo chini ya benchi la ufundi kwa kuwa wachezaji wote wana ari na mechi hiyo.
"Suala la kuanza au kutoanza kwa mshambuliaji, Mosses Phiri hilo ni siri ya benchi la ufundi, kila mchezaji Simba yuko tayari kuitumikia timu, tayari wachezaji wanajua majukumu yao na kazi kubwa ni kuhakikisha tunapata ushindi," alisema kocha huyo Msaidizi wa Simba.
Wakati huo huo Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, alisema kikosi cha Simba kinaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers utakaopigwa kesho.
Alisema kikosi kimeingia kambini baada ya mazoezi ya juzi jioni ya kujiandaa na mchezo huo na kwamba hawahitaji chochote zaidi ya ushindi na kupata pointi tatu ili kujiweka katika nafasi nzuri katika kundi lao.
“Wachezaji wote wameshiriki mazoezi isipokuwa Kibu Denis ambaye amekuwa na programu yake chini ya uangalizi wa daktari kutokana na kupata maumivu katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Uganda.
Morali za wachezaji ipo juu, wanafanya jitihada kubwa mazoezini ili kulishawishi benchi la ufundi kuwapa nafasi katika mchezo wa Jumamne,” alisema Ahmed.
Simba jana walizindua kampeni yao ya kuujaza Uwanja wa Mkapa katika mchezo huo, ambayo ilianza saa 4:30, asubuhi ikiongozwa na Meneja wa Idara ya Habari, Ahmed msafara ukianzia Magomeni Mikumi, kupitia Manzese, Mwananyamala hadi Ufukwe wa Coco, jijini Dar es Salaam, ambayo ilipewa jina la ‘Wenye Nchi Beach Party’.










