Yanga inatarajia kuwakaribisha US Monastir katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Matokeo ya ushindi ndio yataongeza matumaini ya Yanga yenye pointi saba kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, alisema kimbinu timu yao inaendelea vizuri na kila mchezaji anaelekezwa namna ya kutimiza majukumu yake kwa ufasaha katika mechi hiyo muhimu kwao.
Kaze alisema anaamini wachezaji wakitimiza vyema majukumu yao, timu hiyo itazibakisha pointi tatu nyumbani na kuwashangaza wapinzani hao.
Alisema katika mechi ya kwanza walifanya makosa wachache ambayo yaliwagharimu na kubababisha kufungwa mabao mawili ya haraka lakini tayari wameyafanyia kazi na sasa wanaandaa timu itakayowaduwaza Waarabu hao.
"Hatuwaogopi licha ya kufahamu wapinzani wetu wana timu nzuri, walitufunga kwao na sisi tuna uwezo wa kuwafunga hapa Tanzania, tunaendelea kujipanga ili tushinde na naamini tutafanya hivyo kama kila kitu kitaenda kama tulivyopanga," alisema Kaze.
Aliongeza morali ya wachezaji wao iko juu na kilichobakia ni kusubiri muda wa mapambano ambao wamejipanga kucheza kwa umakini ili wasonge mbele katika mashindano hayo.
Mrundi huyo alisema mechi ya Jumapili ni muhimu na inatoa uamuzi wa hatima ya kutinga hatua ya robo fainali huku mpinzani wao na vinara wa Kundi D, US Monastir yenye pointi 10 wakiwa tayari wameshasonga mbele.
Wakati huo huo, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, aliliambia gazeti hili kila mchezaji wa timu hiyo ana ndoto ya kucheza robo fainali na kwa sababu hiyo wamejipanga kucheza kwa kiwango cha juu.
Saleh alisema kipindi cha nyuma timu yao ilikuwa inatolewa katika hatua ya awali ya michuano hiyo ya kimataifa, lakini sasa wana wachezaji wenye uzoefu na ambao wako tayari kuipigania nembo ya Yanga.
“Sisi kwa sasa tunashukuru kwa hamasa hii kutoka kwa Rais Samia, unawaona kabisa wachezaji wanavyopambana ili kuipatia timu matokeo mazuri, tunashukuru kwa kila kitu kinachochangia ushindi wetu.
“Historia imebadilika na wakati huu tunaenda katika mechi ya mwisho wa wiki tukiwa na shauku kubwa ya kuona timu yetu inashinda mbele ya wageni wetu US Monastir," kiongozi huyo alisema.
Baada ya mechi hiyo, Yanga itasafiri kwenda Lubumbashi kuwafuata TP Mazembe katika mechi ya mwisho huku wakiwa na kumbukumbu ya kuwafunga Wakongomani hao mabao 3-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika hapa nyumbani.
Yanga na Simba wanaogelea bahari ya fedha za Rais Samia aliyeahidi kununua kila bao litakalofungwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kwa gharama ya Sh. milioni tano.
Nafasi ya pili katika Kundi D inashikiliwa na Yanga yenye pointi saba ikifuatiwa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), yenye pointi tatu huku Real Bamako ya Mali yenye pointi mbili ikishika mkia katika kundi hilo.










