Simba itawakaribisha Horoya AC kutoka Guinea ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mechi mbili mfululizo za kimataifa dhidi ya Vipers FC ya Uganda na moja ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa ugenini iliwatandika wenyeji, Mtibwa Sugar mabao 3-0.
Robertinho aliliambia gazeti hili kikosi chake kinafahamu kina kazi kubwa ya kusaka ushindi katika mchezo huo kwa sababu wanakutana na timu ngumu.
Kocha huyo alisema mashindano ambayo wanashiriki si mepesi lakini wamejipanga kuvuna matokeo mazuri.
“Wachezaji ambao tunao wengi wana vipaji na uzoefu wa kupambana kutafuta matokeo bora, hakuna ambaye hatambui ubora wa wapinzani wetu (Horoya), lakini ni lazima tuwe na mpango kwa ajili ya kuwakabili.
Tunapaswa kuwabadilishia mipango kulingana na namna ambavyo tutakutana nao, tukiwa katika mazoezi ndipo tunafanyia kazi makosa yetu,” alisema Robertinho.
Aliongeza kila mchezo wanaocheza wanaingia na mpango kazi maalum wenye lengo la kupata ushindi kwa kuzitumia vizuri nafasi za kufunga zinazopatikana na kujihakikisha kuzibakisha pointi tatu.
“Tulipoteza nchini Guinea na Horoya AC, kwa wapinzani wetu kutumia makosa yetu na kufanikiwa kufunga bao 1-0, ninaimani hayawezi kujirudia baada ya kuwepo na mpango mkakati wa kupata ushindi na kucheza hatua ya robo fainali,” alisema Robertinho.
Naye Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema mchezo wa kesho ni muhimu sana kwao na wanawaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Mkapa ili kuwasapoti vijana wao.
"Mchezo wa Jumamosi dhidi ya Horoya AC ni muhimu na mgumu, tunajua kama tutajitokeza mashabiki 60,000 kwa Mkapa, Horoya AC hata wawe bora vipi hawatoki, Wanasimba kutoka kila maeneo yote ya hapa nchini mnatakiwa kujitokeza uwanjani ili timu itinge robo fainali,” alisema Ahmed.
Aliongeza itakuwa fedheha kubwa endapo watashindwa kuifunga Horoya na kuishia hatua ya makundi.










