Yanga: Tunatumbua majipu

08Mar 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Yanga: Tunatumbua majipu
  • Timu hiyo ya Jangwani inashuka kwenye Uwanja wa Taifa leo kuikabili African Sports ikiwa pointi moja nyuma ya vinara Simba.

WAKATI kikosi cha Yanga leo kinashuka kwenye Uwanja wa Taifa kuikabili African Sports, huku uongozi wa mabingwa hao watetezi ukitamba huu ni msimu wao wa "kutumbua majipu kwenye soka".

Wachezaji wa Yanga wakishangilia baada ya kufunga goli walipocheza na Simba hivi karibuni

Ukiziondoa mechi mbili ilizotoka sare dhidi ya Azam FC, timu hiyo ya kocha mkuu Mdachi Hans van der Pljuim imeshinda mechi zingine zote ilizocheza nyumbani jijini Dar es Salaam msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Timu hiyo ya Jangwani inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 47, moja nyuma ya vinara Simba, lakini itaingia uwanja ikiwa na rekodi ya kushinda 1-0 duru la kwanza dhidi ya Sports ambao katika mechi nne zilizopita wameshinda moja, sare mbili na kupoteza moja.

Yanga pia wataingia uwanjani wakijivunia safu yao kali ya ushambuliaji inayoundwa na MTN (Simon Msuva, Amissi Tambwe na Donald Ngoma) ambao kwa pamoja wamefunga mabao 33 katika mechi 20 zilizopita za Ligi Kuu -- Tambwe akifunga 15, Ngoma (12) na Msuva (6).

Sports wanashika nafasi ya pili kutoka mkiani wakiwa na pointi 17, wakifunga mabao saba tu katika mechi 21 zilizopita walizoruhusu nyavu zao kutikiswa mara 21 -- wastani wa kufungwa bao moja kila mechi.

UTUMBUAJI MAJIPU

Jerry Muro, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa msimu huu ni maalum kwa timu yao kufanya vizuri dhidi ya timu ambazo zimekuwa zikiihenyesha kwenye mashindano mbalimbali.

"Huu ni msimu wetu, sisi (Yanga) ni timu ya kimataifa," Muro alisema. "Hao Azam wamesoma alama za nyakati kwamba ubingwa ni wa Yanga na jahazi lao linazama. Badala ya kuomba boya waokolewe, wanakimbilia kulaumu marefa wa mechi.

"Tunatumbua majipu kwenye soka, tumempiga Simba 2-0 duru la kwanza na tumempiga tena hivyohivyo mzunguko wa pili.
"Jumanne (leo) tutarejea kwenye nafasi yetu ya kwanza, tutamtumbua African Sports kisha tunamfuata APR. Tunatumbua majipu hadi barani Afrika."

Raundi ya 22 ya Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea kesho, Tanzania Prisons wakiwakaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku timu za jiji la Tanga, Coastal Union na Mgambo Shooting zikichuana kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Baada ya kuchapwa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Mabatini mwishoni mwa wiki, Mwadui FC watakuwa nyumbani wakiwaalika Majimaji kwenye Uwanja wa Mwadui mkoani Shinyanga, huku Toto Africans wakiwa wageni wa JKT Ruvu mkoani Pwani.

Keshokutwa kutakuwa na mechi mbili, Simba wakipambana na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Taifa, wakati Mbeya City watavaana na Stand United mjini Mbeya.