Mayanja azitisha Yanga, Azam

08Mar 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Mayanja azitisha Yanga, Azam

KOCHA mkuu wa muda wa Simba, Jackson Mayanja, amewapongeza Azam FC na Yanga kutokana na ushindani mkali zinaouonyesha, huku akisisitiza ushindi alioupata juzi dhidi ya Mbeya City FC umefufua matumaini ya timu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Jackson Mayanja

Kikosi cha Wanamsimbazi kilishinda 2-0 dhidi ya City kwenye Uwanja wa Taifa na kukwea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kikiwa na mtaji wa pointi 48 baada ya mechi 21.

Na Mayanja ambaye alipewa jukumu la kuinoa Simba Januari 10 baada ya kutimuliwa kwa Mwingereza Dylan Kerr, alisema matokeo mazuri ya mechi ya juzi yameyaweka hai matumaini yao ya kumalizika ukame wa mataji ya Ligi Kuu uliodumu Msimbazi tangu msimu 2011/12.

"Nawapongeza Azam na Yanga kwa kutupa ushindani mkubwa katika ligi," alisema. "Nawapongeza pia mashabiki wetu kwa kufika kwa wingi uwanjani jana (juzi) kuishangilia timu.

"Wachezaji wanafanya kazi kubwa na kufuata kwa kiasi kikubwa kile ninachowaelekeza, ligi ni ngumu lakini sasa tuko katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa ingawa mechi bado ni nyingi."

Simba itashuka kwenye Uwanja wa Taifa keshokutwa kuikabili Ndanda FC katika mechi ya raundi ya 22 ya ligi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kushinda 1-0 dhidi ya timu hiyo duru la kwanza, Ibrahim Ajibu akiacha huzuni kwa wenyeji kwenye Uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara siku ya kwanza ya mwaka 2016.