Yanga, NMB wazindua kadi zenye bima za mamilioni

09Feb 2024
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga, NMB wazindua kadi zenye bima za mamilioni

KLABU ya Yanga  kwa kushirikiana na Benki ya NMB wamezindua kadi maalum ya wanachama wa timu hiyo iliyopewa jina la ‘NMB, Yanga World Debit MasterCard,’ambayo mwanachama atalipa Sh.milioni moja kuipata, ikiambatana na faida kadhaa ikiwamo bima, seti ya jezi na tiketi 10 za VIP katika msimu mmoja.

Hafla ya uzinduzi wa kadi hiyo ilifanyika jana katika makao makuu ya Benki ya NMB jijini Dar es Salaam, ambako benki hiyo iliwakilishwa na Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, huku Rais wa Yanga, Hersi Said na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Mzambia Andre Mtine wakiwawakilisha 'Watoto wa Jangwani'.

Katika uzinduzi huo uliokwenda sambamba na kukabidhiwa kadi kwa wanachama waliolipia, Mponzi alisema kadi hiyo yenye nembo za NMB, Yanga na MasterCard, itakuwa na faida mbalimbali ikiwamo ukataji tiketi za ndege, bima za upotevu wa mizigo na uahirishwaji safari za ndege.

"Ni kadi yenye faida lukuki, kwa sababu NMB hatujawahi kuja na jambo dogo, hatupoi. Ukishakuwa na kadi hii, utasafiri nayo kote duniani na unafanyia ununuzi na miamala katika sehemu mbalimbali duniani, ikiwamo fursa ya kukaa katika sehemu za watu maalum katika viwanja vya ndege vya kimataifa.

"Pia, NMB Yanga World Debit Black Card ambayo utaipata punde tu utakapofungua akaunti, ukiitumia kukata na kulipia tiketi ya ndege, utaingia moja kwa moja katika bima ya kupotelewa mizigo ambako utalipwa hadi Dola 3,000 (Sh. milioni 7.5), na endapo mizigo itachelewa, bima itakulipa hadi Dola 300.

"Ukinunua tiketi kwa kutumia kadi hii, unapata hadi bima ya Dola 7,500 ambazo ni karibu Sh. milioni 20 ambazo utalipwa endapo safari za ndani na nje ya nchi zitaahirishwa na zaidi ya yote utakuwa sehemu ya huduma za NMB Mkononi na mikopo ukiwamo wa Mshiko Fasta usio na dhamana wala kujaza fomu," alibainisha Mponzi.

Aliongeza ya kwamba kadi hiyo itampa mwanachama wa Yanga punguzo la bei katika ununuzi wa migahawani, ‘supermarket’ na vituo vya mafuta kwa kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi, huku akitoa wito kwa Wana Yanga kujitokeza katika matawi yote nchini kufungua akaunti ama kulipia kadi hiyo.

Naye Hersi mbali na kuishukuru NMB kufanikisha mchakato uliozaa kadi hiyo maalum, aliipongeza kwa mafanikio makubwa iliyopata benki hiyo mwaka jana, ilivuna faida kubwa inayoakisi thamani, ukubwa na ubora wa huduma zao, unaoendana na hadhi ya Yanga.

“Huu ni mwendelezo wa masuala yanayoambatana na sherehe zetu za miaka 89 ya kuzaliwa kwa Yanga utakaofikia kilele Februari 11, tuko hapa kuzindua kadi ya kiwango cha juu kabisa katika huduma za kibenki Tanzania, kadi ambayo inamtambua mtumiaji wake kama mteja wa daraja la juu.