Klabu hiyo pia imesema haitomsajili mchezaji yeyote kwa kelele au presha za mashabiki.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Ali Kamwe, amekiri pia kuwa wamemuuza kiungo Yannick Bangala kwenye Klabu ya Azam FC, huku akisema ukimya waliokuwa nao ulitokana na kumfanyia tathmini mchezaji ambaye walikuwa na mkataba naye.
"Tumemsajili straika huyu kutoka Benchem United FC na ndiye tuliyekuwa tunamfuatilia na si yule Mcameroon ambaye mlikuwa mnamtoa sana kwenye vyombo vya habari na kumfanyia promo, tulikuwa tunafuatilia wenyewe taratibu, hizi promo za hawa wachezaji wengine ambao mlikuwa mnazipiga kuwahusisha na klabu yetu miaka ya nyuma ilikuwa inasababisha klabu zetu kuingia mkenge na kusajili tu kwa sababu ya presha za mashabiki," alisema Kamwe.
Awali, kulikuwa na taarifa kuwa klabu hiyo ingemsajili straika Emmanuel Mahope ambapo ilielezwa kuwa dili lilivunjika dakika za mwisho kwa sababu ya kutaka mshahara mkubwa, lakini kwa mujibu wa Kamwe ni kwamba hawajawahi kuwa kwenye mipango ya kumsajili straika huyo.
Akizungumza kuhusu uhamisho wa Bangala, Kamwe alisema kama klabu wamefanya biashara kwa sababu bado alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja.
"Kwa faida ya mashabiki wote wa soka, wachezaji wenye mikataba ni tofauti sana na wale ambao wamemaliza mikataba kama kina Benard Morrison au Eric Johora wale walikuwa wamemaliza mikataba na ndiyo maana imekuwa rahisi kuwaambia 'thank you', lakini hawa wengine waliokuwa na mikataba zipo hatua za kupitia kwanza.
"Kwanza mchezaji anaweza kusema pamoja ya kwamba nina mkataba wa mwaka mmoja, lakini sitaki kubakia hapa, hivyo klabu inatafuta thamani ya mchezaji halafu ofa zinakuja zinasikilizwa anauzwa, au klabu yenyewe inafanya tathmini na inaamua kumuuza japo ana mkataba, au mnakaa na kukubaliana kuvunja mkataba sasa haya mambo siyo ya kuyafanya kihuni tu," alisema Kamwe akifafanua kwa nini suala hili limechukua muda mrefu kukamilika huku mchezaji huyo na Djuma Shaaban wakitaka kuondoka muda mrefu.
Akimzungumzia Mayele alisema kuwa naye jambo halijakamilika kama lilivyokuwa la Bangala na likishakamilika wataliweka wazi.










