Julai 23, mwaka huu Simba ilitangaza kumsajili kipa huyo kutoka Resende ya kwao Brazil kwa lengo la kuziba pengo la kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula, ambaye anauguza majeruhi yake bega baada ya kufanyiwa upasuaji.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo, zimeeleza suala la kipa huyo limekuwa likifanywa kwa usiri kuwa hatokuwa mmoja kati ya wachezaji wa timu hiyo inayotarajia kuingia nchini kesho kutoka Uturuki baada ya kuvunja mkataba wake kutokana na vipimo vya afya alivyofanyiwa nchini humo.
Aidha, taarifa hizo zimeenda mbali zaidi baada ya kueleza kuwa viongozi wa timu hiyo tayari wameshawasiliana Kocha Mkuu wa timu hiyo, Robertinho Oliveira kwa kumpa majina ya makipa kutoka katika mataifa manne likiwamo Taifa la Slovenia inayopatikana barani Ulaya kwa ajili ya kupitisha jina moja ili kumalizana naye kabla kufungwa kwa dirisha la usajili.
"Jefferson hana uhakika wa kuja nchini kwa sababu amefeli vipimo vya afya na uongozi kwa sasa unapambana kumpata mbadala wake ili kuweza kwenda sawa kabla ya dirisha la usajili kufungwa, unajua kilichosababisha hadi wamkate ni majeruhi ya mara kwa mara na vipimo vimeonesha, ndiyo maana viongozi wanapambana kupata mbadala wake kwa haraka.
"Ni jambo ambalo uongozi umeamua kulifanya siri kwa sababu tayari Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah 'Try Again', alifika juzi nchini Uturuki na kukabidhi majina manne ili kuchagua jina moja la kipa ambaye atakuja kuchukuwa nafasi ya kipa huyo Mbrazili.
"Zoezi hili linatakiwa kukamilika ndani ya siku moja na kesho (leo) kuwahi dirisha la usajili wa CAF ambalo linatarajiwa kufungwa saa 6:00 usiku,” kilisema chanzo hicho makini.
Kwa upande wa Robertinho, alipoulizwa hakutaka kuweka wazi juu ya suala hilo zaidi ya kuongelea kambi ya timu yake ilivyokuwa nchini Uturuki.
"Tumefanyia kazi mambo mengi katika kipindi hiki, ikiwamo utimamu wa miili, umoja, ushirikiano, mbinu na mifumo tutakayoitumia mara kwa mara katika mechi zetu za ndani na kimataifa, kwa wachezaji kuonekana kuelewa kwa haraka zaidi, hayo mengine siwezi kusema chochote," alisema Robertinho.










