Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu Yanga ikiwa uwanja wa nyumbani walikutana na kibarua kigumu na kuvuna alama tatu kwa ushindi wa bao 1-0 dakika za mwisho katika dimba la Azam Complex Chamazi Dar es Salaam.
Kikosi cha Yanga kimeondoka jana kwa ndege kuelekea Nachingwea na hapo watapanda basi moja kwa moja kwenda Ruangwa tayari kwa mchezo huo leo kwenye uwanja wa Majaliwa.
Yanga wanahitaji ushindi katika mchezo huo kwa lengo la kuwaacha mbali kwenye mbio za ubingwa wapinzani wao Azam FC wenye pointi 43 sawa na mabingwa hao watetezi wakiwa mbele kwa michezo mitatu.
Timu hizo zimekutana mara tano tangu mwaka 2021 hadi 2023 na wametoka sare mechi moja ikiwa Novemba 20, 2021 ambapo walifungana 1-1.
Aprili 22 na Desemba 17, 2022 Yanga walishinda mechi zote mbili nyumbani na ugenini, walivuna alama tatu kwa ushindi wa mabao 2-1 na mzunguko wa pili Namungo FC wakiwa nyumbani waliruhusu mabao 2-0.
Februari 4, mwaka jana Yanga walifanikiwa kuvuna pointi zingine wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 2-0 na Septemba 20 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu huu walipata alama zote tatu.
Kuelekea mchezo wa leo Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema maandalizi yameenda vizuri malengo makubwa na kuendelea na safari yao ya kukusanya pointi kila mechi kwa ajili ya kutetea ubingwa.
Amesema mechi hiyo itakuwa ya ushindani mkubwa kwa sababu mechi ya duru la kwanza Namungo FC walionesha mchezo mzuri na kuwapa ushindani mkubwa na kufanikiwa kupata bao dakika za mwisho.
“Tumefanya maandalizi mazuri kukabiliana na Namungo, tunawafahamu mechi ya kwanza walitusumbua na sasa tunaingia kivingine kuhakikisha tunavuna pointi tatu ugenini,” amesema kocha huyo.
Kocha Mkuu wa Namungo, Mwinyi Zahera amesema wachezaji wake wapo tayari kwa mchezo huo kuhakikisha wanatumia vema uwanja wa nyumbani.
“Tumefanya maandalizi mazuri, tunatambua ubora wa Yanga lakini pia wanamadhaifu tutayatumia na kupambana kupata matokeo mazuri mbele ya Yanga,” amesema Zahera.









