Yanga itaikaribisha Mgambo JKT kutoka Tanga katika mechi ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa wakati Azam FC itakuwa wenyeji wa Majimaji ya Songea mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi jijini Dar es Salaam.
Yanga ambayo hatma ya kuendelea kwake kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho itajulikana leo, itawakaribisha Maafande hao kutoka eneo la Kabuku wakikwa na kumbukumbu ya kugawana pointi kufuatia sare ya bila kufungana waliyopata katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani Desemba 12 mwaka jana.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi ya Bara wenye pointi 59 wanahitaji ushindi leo ili kuendelea kuongoza kwenye msimamo ligi wakati Azam FC nayo wanataka kuwakaribia na hatimaye kuongeza presha kwenye mbio hizo za kusaka ubingwa.
Azam FC ambayo tayari imeshatinga fainali ya Kombe la FA leo watashuka kwenye Uwanja wake wa nyumbani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-1 walioupata dhidi ya Majimaji mjini Songea Desemba 20.
Straika wa kimataifa wa Yanga kutoka Zimbabwe Donald Ngoma ametamba kuendelea na kiwango kuwasumbua mabeki wa timu pinzani ili kuisaidia timu yake iweze kupata ushindi katika mechi zote zilizobakia.
"Hakuna mchezo rahisi kwenye mpira, tutawakabili wapinzani wetu (Mgambo JKT) kwa nguvu ile ile tuliyoitumia kwenye mechi zilizopita, mechi ya Coastal Union imeshapita sasa akili yetu tumeelekeza kwenye Ligi Kuu na lengo letu hatutaki kupoteza mechi," alisema Ngoma.
Kocha wa Yanga, Hans van der Pluijm aliliambia gazeti hili kwamba licha ya wachezaji wake kuwa na uchovu kutokana na kucheza mechi nyingi kwa kipindi kifupi, bado wana kila sababu ya kuchukua pointi tatu muhimu katika mchezo wa leo.
"Nilisema kuhusiana na hii ratiba, ila inatubidi kupambana na nashukuru wachezaji wangu umeona hali halisi na wanajua tunahitaji ushindi katika kila mechi," alisema Pluijm.
Naye Kocha Mkuu wa Mgambo JKT, Bakari Shime amesema kwamba wamekuja Dar es Salaam kwa lengo la kutafuta matokeo mazuri.
Shime aliongeza kuwa wachezaji wake wanahitaji kushinda na hatimaye kujiondoa kwenye janga la kushuka daraja kwa sababu nafasi waliyoko kwenye msimamo wa ligi ni mbaya.
Msimamo wa ligi unaonyesha kuwa Yanga wanaongoza ligi wakiwa na pointi 59 wakifuatiwa na Simba wenye pointi 58 na Azam FC wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 55.
Ligi hiyo ya Bara itaendelea tena Jumamosi kwa timu 10 kushuka katika viwanja mbalimbali hapa nchini.










