Endapo Yanga na Azam FC zitashinda mechi zao za leo, basi zitakutana katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo iliyorejeshwa tena msimu huu baada ya kusimama tangu mwaka 2002.
Coastal Union ilifika hatua hiyo baada ya kuifunga Simba mabao 2-1 mchezo uliofanyika Aprili 11 kwenye Uwanja wa Taifa na Mwadui FC iliwaondoa Geita Gold Sport baada ya kupata ushindi wa magoli 3-0.
Yanga leo itashuka kwenye uwanja huo ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha mabao 2-0 walichokipata kutoka wenyeji wao katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara uliofanyika Januari 30 mwaka huu huku pia ikiwa na maumivu ya kuondolewa kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Azam FC inayonolewa na Muingereza Stewart Hall yenyewe itashuka uwanjani Mwadui Complex ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuwafunga Mwadui FC mechi zote mbili za ligi msimu huu na kujipatia pointi sita muhimu.
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm alisema jana mchana kuwa wachezaji wake watatumia uzoefu walionao ili kupata ushindi na hatimaye kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Pluijm alisema kasi waliyotoka nayo Misri, wataiendeleza na hawatakubali kufungwa mara mbili mfululizo na Coastal Union kwenye uwanja huo wa Mkwakwani msimu huu.
"Ni mechi ngumu na yenye changamoto, tunakwenda kucheza tukiwa na bado na joto la mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, kila upande unajua umuhimu wa mechi za mtoano," alisema kocha huyo.
Msemaji wa Coastal Union, Oscar Assenga, aliliambia gazeti hili kwamba timu yake imejipanga imara na katika mechi zote zilizosalia na umoja uliorejea klabuni hapo ndiyo unachangia kupata matokeo mazuri.
"Dhamira yetu ni kuiondoa Yanga kwenye FA ili tuingie fainali na kuchukua kikombe, tuna majeruhi madogo madogo lakini hayawezi kutupunguza kasi yetu, tunajua wameshatumbuliwa na Waarabu sisi tutaendelea kutumbua maeneo mengine yaliyobakia, ” alisema Assenga.
Yanga iliwasili jijini hapa jana mchana tayari kwa mchezo huo wakati Azam FC yenyewe ilitua Shinyanga tangu juzi jioni.










