Sakata la Banda wiki ijayo

24Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Sakata la Banda wiki ijayo

WAKATI kikosi cha Simba kikiwa kambini Zanzibar kujiandaa na mchezo wake wa ligi kuu dhidi ya Azam FC Mei Mosi, Uongozi wa klabu hiyo umesema kuwa utatoa maamuzi wiki ijayo juu ya sakata la mchezaji wake Abdi Banda anayetuhumiwa kwa utovu wa nidhamu.

abdi banda

Banda alitofautiana na kocha wake, Jackson Mayanja na kuamua kumuweka nje ya kikosi hicho kwa muda usiojulikana.

Akizungumza jana, Afisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa sula hilo halijatolewa maamuzi, lakini uongozi umepanga kulimaliza wiki ijayo.

"Suala lake lipo katika ngazi ya maamuzi, uongozi utatoa taarifa wiki ijayo juu ya suala la Banda," alisema Manara. Alisema Simba ni klabu inayofuata taratibu na siku zote itaendelea kuhubili nidhamu kwa wachezaji wa timu hiyo.

"Bila ya nidhamu tutakuwa mbali na mafanikio, Simba ni timu kubwa na ndio maana tunataka wachezaji wetu walinde taswira yake kwa kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja," aliongezea kusema Manara.

Kauri hiyo ya uongozi imekuja siku chache baada ya kumsimamisha beki wake wa pembeni, Hassan Kessy kwa madai ya utovu wa nidhamu ndani ya uwanja.

Banda alitofautiana na Mayanja wakati wa mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Coastal Union Machi 19 baada ya nyota huyo kumgomea kocha wake kuingia uwanjani kuchukua nafasi ya Mohamed Husssein 'Tshabalala'

. Manara alisema kusamehewa au kupewa adhabu kwa Banda itajulikana wiki ijayo baada ya uongozi kutoa maamuzi.

"Alitakiwa kuandika maelezo na tayari amefanya hivyo, uongozi utapitia maelezo yake kabla ya kuamua," aliongeza kusema Manara.

Katika hatua nyingine, Manara, alisema kuwa klabu ya Simba bado haijatoa taarifa rasmi ya kutaka kumchukua kocha Moses Basena ili kusaidiana na Mayanja.

Tangu wiki iliyopita taarifa imezagaa kwenye mitandao ya kijamii Simba kutaka kumchukua Basena. "Hilo suala nimelisikia sana kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, lakini niseme kwa sasa taarifa hizo sio za kweli," alisema Manara.

Alisema kuwa kama kutakuwa na jambo hilo uongozi utatoa taarifa kwa vyombo vya habari ili mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wafahamu.Simba kwa sasa imeweka kambi Zanzibar kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Azam FC.