Watanzania wafunika Kili Marathon

26Feb 2024
Jumanne Juma
MOSHI
Nipashe
Watanzania wafunika Kili Marathon

​​​​​​​MBIO za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zimeendelea kuwa kivutio cha watu wengi kiasi cha kufanya shughuli mbalimbali kusimama katika mji wa Moshi, Kilimanjaro wakati tukio la 22 la mashindano hayo yaliyofanyika jana mkoani humo huku washiriki-

-kutoka Tanzania wakiendelea  kufanya vizuri.

Idadi kubwa ya watu kutoka ndani na nje ya nchi walishiriki katika mbio hizo ambazo zilishirikisha zaidi ya wakimbiaji 10,000, mbio hizo zikijumuisha Kilimanjaro Premium Lager Km 42, Tigo Half Marathon Km 21 na Gee Soseji Fun Run kilometa tano.

Waziri wa Michezo, Utamaduni na Michezo, Damas Ndumbaro,  ndiye aliyeanzisha mbio hizo, ambapo pia alishiriki na kumaliza mbio za kilomita tano za kujifurahisha na baadaye alikuwa kwenye mstari wa kumaliza kupokea washiriki waliomaliza mbio hizo wakiwamo washindi wa vipengele vyote.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Ndumbaro amewapongeza waandaaji wa mbio hizo ambazo alisema zimechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha michezo nchini pamoja na kuibua vipaji vipya kila mwaka.

"Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na waanzilishi wa mbio hizi, pamoja na wadhamini wakuu na wadau wengine wa michezo katika kuhakikisha mbio hizi zilizoanzishwa zaidi ya miaka 20 iliyopita zinakuwa endelevu kwa manufaa ya maendeleo ya michezo nchini.

“Nichukue fursa hii kuwashukuru wadhamini wakuu wa mashindano ya Kilimanjaro Premium Lager na wadhamini wengine ambao ni pamoja na Tigo- Km 21 (Half Marathon), Gee Soseji – Kilomita tano (Fun Run), wadhamini wa meza za maji maeneo wanayopitia wakimbiaji, ambao ni pamoja Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies, Benki ya CRDB,  TPC Sugar, Garda World Security, CMC Automobiles, Salinero Hotels na wauzaji - Kibo Palace Hotel na Keys Hotel," amesema.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa TBL ambao ndio wadhamini wakuu wa hafla hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 2003, Michelle Kilpin, amesema tukio hilo limepiga hatua kubwa wakati likiingia mwaka wake wa 22.

“Mafanikio haya yameshuhudiwa na mamilioni ya watu duniani kote, imekuwa ni safari ya kusisimua kwani haya ni moja ya mashindano makubwa ya kimataifa ya riadha katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki, yanawaleta pamoja zaidi ya wakimbiaji 12,000 na watazamaji wengi zaidi kutoka Tanzania na nje ya nchi ambapo mwaka huu, ilihusisha washiriki kutoka nchi 56,” amebainisha.

Amesema Kilimanjaro Premium Lager imetenga jumla milioni 28/-kama zawadi kwa ujumla.

Katika mbio za Km 42, Augustino Sulle kutoka Tanzania aliibuka mshindi baada ya kutumia saa 02:21:06, mbele ya Abraham Kosgei kutoka Kenya aliyetumia saa 02:22:02 na kushika nafasi ya pili, huku Elisha Kimutai pia kutoka Kenya akitumia saa  02:22:17 na kushinda nafasi ya tatu.

Kwa upande wa wanawake, Natalia Sulle alishinda baada ya kutumia saa 02:51:23 na kushinda mbio hizo, huku akimtangulia Mtanzania mwenzake Neema Sanka aliyetumia saa 02:51:47 wakati Vailet Kidasi akishinda nafasi ya tatu baada ya kukimbia kwa saa 03:01:03 na hivyo kukamilisha ushindi wa Watanzania kwa nafasi zote tatu za kwanza katika kitengo cha kilomita 42.

Katika mbio za Tigo Half Marathon Km 21, kwa upande wa wanaume ushindi ulienda kwa Faraj Damas kutoka Tanzania aliyetumia saa 01:16:40, akifuatiwa na Peter Mwangi kutoka Kenya aliyetumia saa 01:03:44, huku Mtanzania Kennedy Abel akishika nafasi ya tatu baada ya kukimbia kwa saa 01:04:22.

Kwa upande wa wanawake mbio hizo za Tigo Half Marathon, zilizotawaliwa na wanariadha wa Kitanzania, Failuna Matanga alishinda mbio hizo baada ya kutumia saa 01:16:40, Neema Kisuda akashika nafasi ya pili kwa kukimbia kwa muda wa saa 01:16:54, huku Neema Mbua pia kutoka Tanzania akishika nafasi ya tatu baada ya kukimbia kwa saa 01:17:07.

Katika mbio hizo za kilomita 21, Tigo Half Marathon, Vivian Opskvik kutoka Norway alishika nafasi ya tisa baada ya kutumia saa 01:29:09, jambo ambalo lilonyesha msisitizo kuwa mbio hizo ni za kimataifa.