Benchikha achora ramani ya kuimaliza Jwaneng Galaxy

27Feb 2024
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Benchikha achora ramani ya kuimaliza Jwaneng Galaxy
  • Waunganisha kambini, Inonga mgeni rasmi, waamuzi Waghana kuamua, kuziona buku 5...

​​​​​​​BAADA ya Simba kuwasili nchini jana ikitokea Ivory Coast, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha, tayari amechora ramani yake kuelekea mchezo ujao wa mwisho wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo moja kwa moja amewataka wachezaji wake kuelekea kambini -

Abdelhak Benchikha.

-kuanza maandalizi ya mtanange huo.

Simba ambayo mchezo uliopita dhidi ya Asec Mimosas, ilitoka suluhu, sasa inahitaji ushindi wa aina yoyote Jumamosi wiki itakapoikaribisha Jwaneng Galaxy ya Botswana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza na Nipashe, Benchikha amesema hii ni mechi muhimu sana kushinda na kwenda hatua ya robo fainali, hivyo lazima wapambane na kutafuta matokeo mazuri uwanja wa nyumbani.

Amesema kubwa kwake ni kufanyia kazi nafasi wanazozipata na kushindwa kuzibadili kuwa mabao, hususan kuelekea mchezo huo muhimu ambao wanahitaji ushindi ili kufuzu robo fainali ya michuano hiyo kwa mara nyingine.

Benchikha amesema mechi yao na Asec Mimosas walicheza vizuri sana, lakini walishindwa kutumia nafasi iliyopatikana kupitia kwa Sadio Kanoute, ambayo ingekuwa muhimu sana kwao.

“Tunasahau hilo, tumerejea nyumbani kusahihisha makosa yetu, kundi ni gumu sana, lakini kwetu tunataka kushinda mechi yetu ya Jwaneng Galaxy kwa sababu itatuwezesha kufuzu kucheza robo fainali kwa mara nyingine.

"Tunajua historia ya wapinzani wetu miaka ya nyuma, lakini haihitaji kuiweka akili zaidi ya kuandaa timu na wachezaji  kutumia nafasi wanazotengeneza kutafuta ushindi,” amesema Benchikha.

Nahodha wa Simba,  Mohammed Hussein, amesema wamerejea nyumbani na wanaingia kwenye mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy kwa tahadhari kubwa kulingana na kuwafahamu wapinzani wao hao.

“Hii ni mechi ngumu sana na muhimu kwa Wanasimba wote kujitokeza uwanjani kwa sababu inatoa hatima yetu ya kwenda kucheza robo fainali kwa mara nyingine.

"Tunawakumbuka sana Jwaneng Galaxy kwa kilichotokea Uwanja wa Benjamin Mkapa 2021, hatutafanya makosa tena na tunahitaji kushinda mechi hii ambayo itatupeleka hatua ya robo fainali, lakini tunataka kulipa kisasi,” amesema nahodha huyo.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, amesema mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy itachezwa Jumamosi saa 1:00 usiku, kwa sababu ya maelekezo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kutaka ipigwe muda huo sawa na ile Wydad Casablanca dhidi ya Asec Mimosas.

Amesema kikosi kimerejea nyumbani na kinaingia kambini moja kwa moja kuendelea na maandalizi ya kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Soka nchini, maarufu FA Cup dhidi ya TRA utakaochezwa keshokutwa, Jumatano.

“Timu imerejea na kuingia kambini kujiandaa na mchezo huo pamoja na mechi ya kimataifa dhidi ya Jwaneng Galaxy ambao tutacheza Machi 2, mwaka huu, bado hatujapata taarifa ya lini wapinzani wetu wanakuja licha ya baadhi ya watu wao kufika nchini.

"Huu ni mchezo muhimu sana kushinda, kutafuta ushindi wa aina yoyote, hatusubiri kuangalia mechi ya Wydad Casablanca dhidi ya Asec Mimosas. Kama tukishinda tunatimiza alama tisa hali kadhalika Wydad wakishinda wanakuwa na pointi sawa na sisi.

"Lakini Simba itaenda kwa sababu ya kanuni kwa kuwa tulipokutana na Wydad Casablanca walitufunga kwao bao 1-0 na walipokuja hapa tukawafunga mabao 2-0 hiyo itatufanya twende kwa mara ya tano robo fainali,” amesema Ahmed.

Amesema kila Mwanasimba aliyefanikiwa kuifanya timu yao kuvuna alama sita katika makundi, sasa wajitokeze kwa wingi Jumamosi uwanjani kuhakikisha wanatinga hatua ya robo fainali kwa mara ya tano.

“Hii Jwaneng Galaxy tunaikumbuka sana 2021, walitusababishia maumivu makubwa ambayo hayajasahaulika kwa Wanasimba, sasa wamekuja kwetu tumejipanga kulipa kisasi kwa siku ya Machi 2, huu ni muda wa wao kuwapa mateso,” amesema.

Ameeleza kuwa safari hii katika mchezo huo una mambo mawili kwanza ni kutafuta ushindi na pili kulipa kisasi kwa Jwaneng Galaxy, na kwamba hamasa kuelekea mechi hiyo itaanza kesho, Jumatano eneo la Keko, wilayani Temeke, Dar es Salaam.

"Mgeni rasmi wa mchezo wetu ni beki, Henock Inonga, ambaye ni mchezaji pekee ameipeleka timu yake ya taifa kucheza mshindi wa nne wa michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon)," amesema Ahmed.

Kuhusu waamuzi wa mchezo huo amesema wanatarajia kutumia nchini Februari 29, mwaka huu, wakitokea nchini Ghana, ambao ni  Daniel Jim Ayi Laryee, Kwasi Acheampony Brobbey, Roland Nii Dondoo Addy na Charles Banle Bulu.

Ahmed pia ametangaza viingilio vya mchezo huo kuwa mzunguko ni Sh. 5,000, VIP C  Sh. 10,000,  VIP B Sh. 20,000, VIP A Sh. 30,000,  Platinum Sh. 150,000 na safari hii kuna tiketi za Tanzanite ambazo ni Sh. 200,000, hizo zikiwa ni kwa watu maalum ambao watakaa karibuni na viongozi watakaojitokeza uwanjani.