Waogeleaji wanne Bongo wafuzu kwenda Dubai

15Mar 2016
Nipashe
Waogeleaji wanne Bongo wafuzu kwenda Dubai

CHAMA cha Kuogelea Tanzania (TSA) kimetangaza majina ya waogeleaji wanne watakaokwenda Dubai kushiriki mashindano ya kusaka viwango vya kushiriki kwenye michezo ijayo ya Olimpiki.

Michuano hiyo ya kusaka viwango imepangwa kufanyika Machi 29 hadi Aprili 7 kwenye viwanja vya michezo vya Hamdan (Hamdan Sport Complex) nchini Dubai.

Katibu wa TSA, Ramadhan Namkoveka, jana aliwataja waogeleaji hao kuwa ni Hilal Hilal, Collins Saliboko, Aliasgher Karimjee na muogeleaji wa kike Sonia Tumiotto.

Alisema mbali na mashindano ya kuogelea, siku hiyo kutakuwa na michezo tofauti ikiwqamo ya kuchezea mpira kwenye maji (water polo), ambayo itaanza siku ya ufunguzi.

Alisema waogeleaji hao wamepata nafasi hiyo baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya taifa ya kuogelea yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Machi 5.

Kiongozi huyo aliwaomba wadau wa michezo nchini kuisaidia TSA kupata Sh milioni 21 ambazo zinahitajika kwa ajili ya safari ya Dubai ya waogeleaji hao.