Wanalambalamba waliibuka na ushindi huo mnono ugenini jijini Johannesburg katika mechi yao ya kwanza ya raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Lakini timu hiyo sasa iko pointi saba nyuma ya vinara wa ligi ya Bara, Simba ambao hata hivyo, wamecheza mechi tatu zaidi.
Na katika kuhakikisha wanapunguza pengo la pointi, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Mario Marinica, alisema jana kuwa wanatakiwa kuwa "waangalifu" katika mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam FC jijini Dar es Salaam.
Kocha huyo alisema wataangalia wachezaji walio tayari kwa mchezo huo ambao alisisitiza wanapaswa kushinda ili kuyaweka hai matumaini yao ya kutwaa taji la pili la Ligi Kuu.
Kocha huyo pia aliendelea kuponda viwango vya marefa wa soka wa Tanzania ambao alidai wamekuwa changamoto kubwa kwa mafanikio ya timu yake.
“Watu wanaweza kujiuliza kwa nini Azam FC haionyeshi kiwango kile kizuri Tanzania (walichokionyesha Afrika Kusini), nilisema awali kuwa Tanzania, Azam FC haitakiwi ichezee sana mpira kwa sababu ya waamuzi, wanafanya vitu vya aibu uwanjani, hivyo hatuwezi kucheza aina ya soka tunalotaka kucheza," alisema.










