Wamisri kutua leo, Yanga wajifua vikali

06Apr 2016
Somoe Ng'itu
Dar
Nipashe
Wamisri kutua leo, Yanga wajifua vikali
  • ***Mabingwa hao wa Bara jana walianza programu maalumu ya mazoezi ya kujenga stamina ili kwenda sambamba Al Ahly…

WAKATI wapinzani wa Yanga Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri wakitarajia kutua nchini leo, mabingwa hao wa Bara jana walianza programu maalum ya mazoezi ya kujenga nguvu, tayari kuivaa kwa mchezo wa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kiungo wa Yanga, Haroun Niyonzima akizuiwa na Beki wa Al Ahly ya Misri, katika mchezo uliopita.

Al Ahly, mabingwa wa kihistoria wa michuano ya Klabu Afrika, wanawasili asubuhi tayari kwa mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka.

Yanga inalazimika kuandaa programu ya kujenga stamina baada ya kuwasoma wapinzani wao wanaotumia nguvu nyingi na kasi.

Kocha Hans van der Pluijm alisema jana kuwa wachezaji wake walifanya progamu hiyo maalum kwenye fukwe.
Pluijm anaamini soka ni akili na nguvu pia, hivyo ili kujenga kikosi imara chenye uwezo wa kucheza dakika 90 bila kuchoka, lazima kuwa na program maalum.

"Tunajua Al Ahly wanavyocheza, lazima tuwe vizuri kila idara. Unapoindaa timu iliyokamilika kila idara ndiyo unavyokuwa jirani na kupata mafanikio,” alisema Pluijm.

Alisema mbali na mazoezi hayo maalum, pia hutumia muda kuangalia kwenye video baadhi ya mechi walizocheza wapinzani wao.

"Unapopata matokeo mazuri nyumbani, utakuwa umevuka kikwazo cha kwanza, hayo ndiyo malengo yetu. Tuna uwezo wa kuiondoa Al Ahly," alisema Pluijm.

Alitoa mfano mechi yao ligi dhidi ya Kagera Sugar, Yanga ilistahili kupata ushindi wa mabao 6 au 7, lakini hiyo ilishindikana kwa kutokuwa makini.

Yanga ambayo itarejea jijini Ijumaa jioni, itamkosa kiungo wake wa kimataifa, Haruna Niyonzima aliyebaki Dar es Salaam kutokana na kusumbuliwa na homa ya malaria. Baada ya mechi ya Jumamosi, Al Ahly wataikaribisha Yanga Aprili 20 mjini Alexandria.