Azam FC kujiuliza kwa Ndanda

06Apr 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Azam FC kujiuliza kwa Ndanda

BAADA ya kung'ang'aniwa na sare ya bao 1-1 na Toto Africans ya Mwanza wikiendi iliyopita, Azam FC leo wanaendelea na ratiba ngumu ya mechi za viporo kwa kucheza dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Uwanja, Chamazi Dar es Salaam.

kocha wa azam, Stewart Hall.

Awali, Azam walililiomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuisogeza mbele mechi hiyo ili wapate muda wa kujiandaa na mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia mwishoni mwa wiki hii.

Hata hivyo, TFF kupitia Bodi ya Ligi ilikataa maombi hayo, hivyo kuilazimu Azam kuendelea na ratiba hiyo.

Kocha Stewart Hall, ameonekana kuupa umuhimu mkubwa mchezo huo kutokana na kutoridhishwa na matokeo ya mchezo uliopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Hata hivyo, katika mchezo wa leo, Hall atamkosa beki wake Shomari Kapombe, ambaye anasumbuliwa na malaria, lakini Michael Gadiel anatarajiwa kuziba nafasi hiyo, huku winga Mcha Hamis, akiendelea kupewa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza baada ya kuonyesha kiwango kizuri kwenye mchezo uliopita.

Kipa Aishi Manula ataendelea kusimama kwenye nguzo mbili za Azam, huku Jean Mugiraneza, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Michael Bolou wakiweka ukuta wa viungo kwa mfumo unaopendwa na Hall wa 3-5-2.

Washambuliaji John Bocco na Kipre Tchetche watakuwa mbele kusubiri mipira kutoka kwa viungo ili kutikisa nyavu.
"Hakuna mechi rahisi, tutashuka uwanjani kwa ajili ya kusaka ushindi, mazingira ya mechi iliyopita jijini Mwanza hayakuwa mazuri, tumerudi kwenye uwanja tuliouzoa," alisema Hall.

Kocha wa Ndanda FC, Abdul Mingange alisema anatambua kwamba anakwenda kucheza dhidi ya timu yenye uwezo, hata hivyo amejipanga kupata ushindi kwenye mechi hiyo.

Simba iliyocheza mechi 24, inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 57, Yanga katika nafasi ya pili kwa pointi 53 na Azam inashika nafasi ya tatu kuwa kuwa na pointi 51.