Taarifa iliyotolewa jana na klabu hiyo, imeeleza kuwa wameingia mkataba wa mwaka mmoja na mchezaji huyo akitokea Azam FC, ikiamini atakuwa msaada mkuba kwenye kikosi hicho.
"Tuna furaha kuwataarifu kuwa tumeingia mkataba wa mwaka mmoja na Tepsi Evance akitokea Azam FC mwa mkopo," ilieleza taarifa hiyo.
KMC inaonekana kufanya usajili mkubwa kuelekea msimu ujao wa ligi baada ya kutofanya vema msimu uliopita.
Tayari imeshawasajili Rogers Gabriel kutoka Pamba na Juma Shemvuni, Wibol Maseke aliyeachwa na Azam FC, Rahim Shomari na Andrew Sinchimba, ikimtwaa pia straika Ibrahim Elias raia wa Somalia kutoka Klabu ya Kibra United ya Kenya.
Hivi karibuni, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Christina Mwagala, alisema kuwa kimetengwa kiasi cha Sh. bilioni moja kwa ajili ya usajili wa msimu unaokuja na hawatosajili mchezaji yeyote ambaye ameachwa na klabu yake.
"Mkurugenzi wetu mama Hanifa Selemani Hamza, ametenga kiasi cha Sh. bilioni moja kwa ajili ya kufanya usajili, maisha magumu tulioyapitia kwa misimu miwili iliyopita haikuwa rafiki kwetu, lazima tufanye usajili wa maana na kwa pesa hizi KMC hatusubiri wachezaji makapi, sijui nani kaachwa ndiyo tuende kumsajili.
"Msimu huu hatuchukui wachezaji ambao wameshindwa kufanya vizuri walikotoka, badala yake ni wapya kabisa kwenye macho ya mashabiki wa soka nchini na wengine tutawavunjia mikataba kwenye klabu zao na kuwasajili," alisema.
Wakati huo huo, KMC juzi ilicheza mechi ya kujipima nguvu dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na kushinda mabao 6-4 kwa mikwaju ya penalti, baada ya sare ya bao 1-1 dakika 90 za mchezo.










