Akiwaaga wanachama na mashabiki wa Yanga, Mayele alisema ana imani bila yeye, Yanga inaweza kufanya vema kwani wamesajili wachezaji wazuri, lakini akikumbuka mazuri yote, mafanikio na nyakati za furaha walizokuwa nazo pamoja.
"Leo nataka nitoe shukrani zangu, maamuzi niliyoyachukua ni magumu, lakini sina jinsi ya kufanya, nimekuja hapa mmenipokea vizuri nilikuwa naishi kama kwetu tu Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, natoa taarifa kwamba nakwenda kutafuta changamoto nyingine.
"Nimekaa sana kwenye vikao na viongozi, wamepambana sana kutaka kunibakisha, wametumia kila aina ya uwezo wao kunishawishi nibaki, lakini na mimi nikawaambia waniruhusu tu niende kutafuta changamoto nyingine nje ya hapa, najua Yanga ni nyumbani, kuna leo, kesho na keshokutwa naweza kurudi kwa sababu hii imeshakuwa ni familia yangu na wao hawawezi kuniacha," alisema mchezaji huyo ambaye mbali na kuwa straika namba moja wa timu hiyo, lakini alikuwa maarufu kutokana na aina yake ya ushangiliaji iliyopendwa na wengi.
Mayele pia alikumbushia nyakati ambazo zilikuwa za furaha kwa wanachama na mashabiki ambazo zitamfanya kuikumbuka klabu hiyo na watu wake kwa ujumla.
"Natoa shukrani zangu za dhati kwa Klabu ya Yanga kwa sababu tulikuwa wote kwa misimu miwili ambayo ilikuwa mizuri sana, tulifurahi sana, tumechukua mataji sita kwa misimu hiyo na tumeweza kuipeleka timu fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika na tumepambana kweli kweli pamoja na viongozi, benchi la ufundi, wanachama na mashabiki pia, nakumbuka mechi dhidi ya US Monastir mvua ilinyesha kweli, lakini mashabiki walijaa uwanjani na tukashinda," alisema.
Aidha, alikiri kuwa kulikuwa na baadhi ya nyakati ngumu, lakini viongozi wa klabu hiyo wakiongozwa na rais wa Klabu, Injinia Hersi Said, walikuwa karibu nao kutatua changamoto yoyote, akimtaja rais huyo kuwa alikuwa nao muda wote na sehemu zote wanazokwenda.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo, Alex Ngai, alisema viongozi wa Yanga walifanya kila njia ikiwamo kuongeza dau, lakini ilifika mwisho wakanyanyua mikono kutokana na timu zilivyokuwa zikipanda kila wao wanavyotaka kumbakisha.
Alikiri kuwa klabu za Afrika Kaskazini maarufu kama za Waarabu hazishindwi kuchukua mchezaji yeyote chini ya Jangwa la Sahara kutokana na kuwa vizuri zaidi kiuchumi.
"Ilikuwa vita, sisi tukipanda dau la usajili na mshahara na wenzetu pia wanapanda, imekwenda hivyo mpaka tukashindwa, hizi timu za Afrika Kaskazini zina uchumi mkubwa zikitaka mchezaji hazishindwi kumpata," alisema Ngai.
Alisema si Pyramids tu ilikuwa ikimhitaji bali zilikuwapo zingine ikiwamo moja kutoka nchini Qatar, lakini Mayele mwenyewe alichagua kwenda Misri kwa sababu anaamini kuna ushindani na ligi bora.
Mayele alitambulishwa rasmi juzi usiku kuwa mchezaji wa klabu hiyo nchini Misri ambayo msimu uliomalizika ilifika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.










