Tangulia 'mfalme' Jumbe, umejitahidi kuchechemea

12Apr 2023
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tangulia 'mfalme' Jumbe, umejitahidi kuchechemea

NI mwishoni mwa miaka ya 90 alipozushiwa kifo, hadi akaamua kutunga wimbo wa 'Nachechemea' wakati huo akiitumikia bendi ya Mlimani Park Orchestra, wimbo ambao hadi sasa haujachuja.

Huyu si mwingine bali ni mwimbaji Hussein Jumbe, ambaye alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Amana, Ilala jijini Dar es Salaam na mazishi yake yalitarajiwa kufanyika katika makaburi ya Kisutu jana.

Mwimbaji huyo aliyekuwa na tungo nyingi zenye hisia kali na za visa vingi vya kweli, amefariki huku tungo yake ya mwisho ikiwa ni 'Hasama'  iliyoachiwa hewani mwishoni mwa mwaka jana akiwa na bendi ya Mlimani Park Orchestra baada ya kuachana na bendi yake ya Talent.

Wakati wa uhai wake, aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa 'Nachechemea' ni wimbo unaotokana na kisa cha kweli, hasa alipougua kwa muda mrefu na kuambiwa kwamba anasumbuliwa na UKIMWI kisha akazushiwa kifo.

Baada ya kupona na kurudi kazini katika bendi yake ya Mlimani, ndipo akafyatua kibao hicho, ili kuonyesha umma wa mashabiki wa muziki wa dansi kuwa yupo na anaendelea kuchechemea.

Wimbo huo ulipendwa na watu wa kada mbalimbali, akiwamo aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mzee Yusuf Makamba, ambaye shughuli za kiserikali akiona bendi hiyo ipo, aliomba kuimbiwa wimbo huo.

Moja ya kauli zake ambayo alikuwa akiirudia mara kwa mara, katika mazungumzo yake, ni kuhusu kisa cha kutunga wimbo wa 'Nachechemea' aliugua sana na kwamba aliponusurika kifo, asingekufa mapema.

Hata hivyo, amefariki dunia ikiwa imepita zaidi ya miaka 20 tangu alipozushiwa kifo kilichomfanya atunge wimbo huo, unaoendelea kupigwa na bendi ya Mlimani Park, huku sehemu ikiimbwa na Hassan Kunyata.

Katika uhai wake, amewahi kuelezea baadhi ya changamoto alizokutana nazo, ikiwamo kuumwa mara kwa mara magonjwa ya mauzauza, lakini kali zaidi ikiwa ni pale alipoota anapigana na kuku hadi kuvunjika vidole vinne.

Jumbe ameondoka akiwa ameacha umaarufu mkubwa kwenye muziki wa dansi kutokana na tungo zake katika bendi mbalimbali alizowahi kuzitumia kabla kujiunga na Sikinde Original, iliotoka ubavuni mwa Mlimani Park.

Baadhi ya tungo zake ni 'Siri ya Nini, Isaya, Huruma kwa Wagonjwa wakati akiwa TOT-Plus, kisha akaurudia wimbo huo akiwa Mlimani Park na kuupa jina la Huruma kwa Wagonjwa na Kilio cha Swahiba'.

Nyimbo nyingine za mkongwe huyo wa muziki wa dansi ni 'Epuka No. 2,  Nuru ya Upendo, Shamba, Mtoto wa Mitaani, Chozi la Kejeli', ambazo ni wazi kila mmoja ulitamba kwa wakati wake.

Jumbe aliyewahi kupachikwa majina mengi yakiwamo ya 'Mzee wa Dodo, Mtumishi' na mengine, amewahi kufanya kazi katika bendi kadhaa, miongoni mwake zikiwa ni Urafiki Jazz, Tabora, Msondo Ngoma, Mlimani Park, TOT-Plus na Mikumi Sound ya mjini Morogoro.