Baleke ambaye alifunga mabao mawili wakati wakishinda 2-0 juzi katika Uwanja wa Highland Estates, Ubaruku, Mbarali mkoani Mbeya kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu FC, amekuwa akidaiwa kuwa yupo Simba kwa mkopo na mwishoni mwa msimu Klabu yake ya TP Mazembe imeeleza nia yake ya kumrejesha.
Hata hivyo, uongozi wa Klabu ya Simba umeliambia Nipashe jana kuwa ina mkataba naye hadi Desemba 2024 na wala hayupo kwa mkopo kama baadhi ya watu wanavyodhani.
Straika huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amewafunga Ihefu mabao matano ndani ya siku chache, kwani Ijumaa iliyopita aliifunga mabao matatu 'hat-trick' kwenye mechi ya Kombe la FA iliyopigwa, Uwanja wa Azam Complex, Simba ikishinda mabao 5-1.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amezima minong'ono kuwa mchezaji huyo yupo kwa mkopo, akisema Simba imempa mkataba wa miaka miwili ambao utamalizika Desemba 2024.
"Desemba mwaka jana tumemsainisha kutoka TP Mazembe kwa mkataba wa miaka miwili, kutoka Desemba hadi sasa ni miezi minne tu, kwa hiyo katika mkataba wa miezi 24, Baleke ametumia miezi hiyo tu, hivyo amesalia na miezi 20 mkononi, wanachama na mashabiki wa Simba watulie, waendelee kufurahia mema ya straika huyo.
"Uwapo wake na wale wenye wasiwasi kukutana naye kiasi cha kupiga simu asubuhi mchana na usiku TP Mazembe kumuulizia Baleke, tuwaambie tu kuwa ni mchezaji wetu kwa miaka miwili, rasmi leo Klabu ya Simba tunaweka wazi kuwa tuna mkataba naye wa miaka hiyo na wala si kwa miezi sita kama wengine wanavyodai, tulisaini naye mkataba kutoka Desemba 2022, ambao utaisha Desemba 2024," alisema Ahmed.
Kwa upande wa Baleke akizungumza na gazeti hili jana, alisema bado hajaanza kuzoea vizuri ligi na ana imani kila muda unavyozidi kwenda na kupata nafasi ya kucheza ndani atazidi kuwa bora.
Alisema kufunga ni jukumu lake kila anapopata nafasi ya kufanya hivyo na kwamba wanacheza watu wengi uwanjani, hivyo akiona mchezaji mwenzake yupo nafasi nzuri ya kufunga anatoa pasi.
“Tunajua wote tunajenga Simba moja, hutakiwi kuwa mchoyo, mchezaji mwenzako anapokuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kuisaidia timu kupata ushindi unamsaidia kwa sababu ninaamini tuliokuwapo hapa tunahitaji kufikia malengo," alisema.
Alisema anaamini kwa sasa tayari ameanza kuzoea mfumo na bado anahitaji muda kidogo wa kuendelea kuzoea mazingira ya ligi ya Tanzania, hivyo anatarajia msimu ujao kwake na Simba utakuwa mzuri zaidi.
Aliongeza kwa sasa nguvu kubwa ni kuangalia yaliyopo mbele hususan mechi zilizosalia katika ligi ikiwamo mchezo wa 'dabi' dhidi ya Yanga Jumapili wiki hii, Kombe la Shirikisho na kazi kubwa kwao ni kuelekea mchezo wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco.
“Mbele yetu tuna kazi nyingi, tunapaswa kuelekeza nguvu kupambana kwa pamoja kwa kushinda mechi zetu zijazo dhidi ya Yanga, kutinga hatua ya nusu fainali ya CAF na tunapaswa kuongeza ushindani zaidi tufanikiwe, malengo yetu hayo,” alisema Baleke ambaye ameanza kuzua hofu kwa wapinzani hasa kwa kasi yake ya kufunga.
Baleke aliyesajili Simba kipindi cha dirisha dogo msimu huu, hadi sasa amefunga mabao 14 tangu ajiunge na timu hiyo, huku akiwa amefikisha saba kwenye Ligi Kuu mpaka sasa, matano kwenye Kombe la FA na matatu Ligi ya Mabingwa Afrika.
Imeandikwa na Saada Akida na Adam Fungamwango










