Tamasha la Access 2023 kufanyika kesho

07Nov 2023
Faustine Feliciane
Dar es salaam
Nipashe
Tamasha la Access 2023 kufanyika kesho

KONGAMANO Kubwa la Kimataifa la muziki la Acces linatarajiwa kufanyika kesho katika ukumbi wa Mliman City jijini Dar es Salaam.

Katibu wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Dk Kedmon Mapana

Kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na wasanii na wadau wa muziki zaidi ya 2,000 kutoka katika nchi mbalimbali Afrika huku likienda sambamba na tamasha kubwa la muziki.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Katibu wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Dk Kedmon Mapana, amesema Serikali inashirikiana kwa karibu na Taasisi ya Music in Africa wanaoendesha kongamano hilo.

Amesema kongamano hilo linatarajiwa kuhusisha wasanii, waandaaji wa muziki, wamiliki wa lebo na wadau wa muziki.

Ameongeza kongamano hilo linafanyika nchini kwa mara ya pili, ambapo lengo lake ni kuhakikisha linawaweka wasanii na wadau mbalimbali kuhakikisha wanafikia malengo ikiwemo kuuza kazi zao katika mitandao na nje ya nchi.

“Serikali chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Taasisi ya Music in Africa tumeandaa kongamano la wasanii litakaloambatana na burudani, lengo ni kuapa wasaa wetu fursa ya kujifunza na kujitangaza zaidi kimataifa," amesema Dk Mapana.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Music In Africa, Eddie Hatitye, amesema kongamano hilo litahusisha wadau wakubwa na kuwakusanya pamoja wasanii mbalimbali kutoka Afrika.

Amesema kongamano hilo litasaidia wasanii kutengeneza mahusiano ya karibu na wadau mbalimbali wa muziki ili kunufaika na kazi wanazozifanya kila siku.

Amesema mara baada ya Kongamano hilo, kutafanyika tamasha kubwa kla muziki ambapo wasanii mbalimbali watapanda jukwaani kuimba.

“Kongamano pia litahusisha wasanii wa muziki wa singeli kwa mara ya kwanza mwaka huu kutokana na kuwa na mashabiki wengi, lengo ni kutengeneza mahusiano mazuri baina ya wasanii na wadau mbalimbali ikiwa pamoja na kubadilishana mawazo, kupata elimu na kufanya biashara kwa pamoja,” amesema Hatitye.

Amesema baadhi ya wasanii watakaopanda jukwaani ni pamoja na Christian Bella, Mario, Sho Madjozi na wengineo kutoka nchi mbaloimbali.

Tamasha hilo linatimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake na limeshafanyika katika nchi za Afrika Kusini, Ghana, Kenya na Tanzania linafanyika kwa mara ya pili mfululizo.