Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, kikosi chake kitaingia kivingine kuwakaribisha wapinzani wao, Raja Casablanca kwa sababu wanahitaji ushindi na si matokeo mengine tofauti.
Robertinho alisema aina ya uchezaji ya ugenini na nyumbani huwa na tofauti kubwa, hivyo wamejiandaa kushambulia zaidi na amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo.
Kocha huyo alisema anataka kuona vijana wake wakicheza kwa kasi kubwa dakika zote 90 ili kuhakikisha wanazibakisha pointi tatu nyumbani.
Alieleza walipocheza dhidi ya Horoya AC aliwataka wachezaji kujilinda na kushambulia kidogo na baada ya kufungwa bao pekee katika mchezo huo walifunguka kwa kuwashambulia wenyeji ili kusaka goli la kusawazisha.
“Nimepanga kuifanyia maboresho safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Moses Phiri, John Bocco, Jean Baleke, Pape Sakho, Clatous Chama na Kibu Denis ili kuhakikisha wanapata ushindi wa mabao mengi nyumbani. Nataka kuona wachezaji wangu wakilishambulia goli la mpinzani wetu mara nyingi zaidi kwa maana ya kuanzia dakika ya kwanza hadi 90, kila mchezo wa nyumbani,” alisema Robertinho.
Alisema hatua waliyofika katika mashindano hayo kila timu inatakiwa kupambana kupata ushindi nyumbani na kutafuta sare ugenini.
"Tunahitaji matokeo ya ushindi katika mchezo dhidi ya Raja Casablanca, kupata matokeo hayo tutalazimika kuingia na mbinu tofauti na tulivyoingia kwenye mechi iliyopita," Robertinho alisema.
Wakati huo huo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema klabu yao jana iliwapokea maofisa kutoka CAF kwa ajili ya ukaguzi wa miundo mbinu kuelekea michuano ya Super League.
“Maofisa hao watakagua maeneo yote muhimu yanayohitajika kwa ajili ya michuano hiyo kama viwanja vya mazoezi, uwanja wa mchezo pamoja na hoteli. Uongozi wa klabu umewapa ushirikiano mkubwa ili kukamilisha kazi yao kwa haraka kwa muda unaotakiwa," aliongeza Ahmed.
Kuelekea mechi dhidi ya Raja Casablanca, Ahmed alisema wataingia kwa tahadhari katika mechi hiyo, ingawa haamini kama wapinzani wao watabadilisha mfumo ambao wamezoea kuucheza.
"Tahadhari ni muhimu, mchezo ni mgumu, ila sisi tunakwenda kutafuta matokeo mazuri, tunajua mpira wa barani Afrika umebadilika, lakini timu za Afrika Kaskazini ambazo tunaziita za Kiarabu hadi leo bado hazijabadilisha mfumo wao wa uchezaji, bado kwa kiasi kikubwa sana wanategemea kushinda kwenye viwanja vyao vya nyumbani, Al Ahly, pamoja na ubora wake wote, huwezi kuona ubora wake wa asilimia 100 wakiwa viwanja vya ugenini, labda kama ametanguliwa kufungwa ndiyo unamwona anaanza kufurukuta na kututumka.
Akirudisha bao anarudi tena kwenye aina yake ya uchezaji wa taratibu na kupoteza muda, mechi yake anayotegemea ni ile ya nyumbani. Hivyo hivyo kwa Raja Casablanca, hatutegemei kama anaweza kuja hapa akacheza kwa kasi kubwa kama anavyocheza kwao, lakini vyovyote itakavyokuwa sisi Simba tumejidhatiti iwavyo ilivyo, tuhangaike naye kuanzia dakika ya kwanza hadi 90 kwa kasi ya hali ya juu, tumepelekee moto kweli kweli, mwisho wa siku tupate pointi tatu," alisema Ahmed.
Simba ambayo ipo katika Kundi C, inakwenda kucheza mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Horoya ya Guinea, wakati vinara wa kundi hilo wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kuitwanga Vipers SC ya Uganda mabao 5-0










