Yanga inatarajia kuikaribisha TP Mazembe katika mechi ya Kundi D itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, alisema timu yake itashuka dimbani kucheza mechi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na njaa ya mafanikio.
Nabi alisema wamejiandaa kisaikolojia kuhakikisha wanapata matokeo chanya ili kufikia malengo ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Kocha huyo alisema wanafahamu mechi hiyo haitakuwa nyepesi kwa pande zote mbili lakini wana matumaini watatumia vizuri uwanja wa nyumbani.
“Sioni kama tunastahili kufanya makosa kama yale tuliofanya Tunisia, tunajua mechi haitakuwa rahisi, tunakwenda kukutana na timu nyingine bora lakini tunapaswa kucheza kama Yanga yenye njaa ya mafanikio, wao wametoka kushinda mchezo wa kwanza, hivyo ari yao itakuwa juu,” alisema Nabi.
Kocha huyo aliongeza amewaangalia vizuri TP Mazembe katika mechi zake mbalimbali na kuona ubora pamoja na madhaifu yao, hivyo atahakikisha anafanyia kazi ili kufanikisha malengo ya timu yake.
Aliongeza hawatarajii kurudia makosa waliyofanya katika mchezo wa kwanza uliochezwa ugenini Tunis ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi mipira ya Set Pieces ambayo walifungwa na US Monastir.
Kuhusu beki wao mpya, Mamodou Doumbia, alisema sio kila mchezaji anayesajiliwa na timu hiyo ataingia katika kikosi moja kwa moja na badala yake anahitaji 'kumpika' taratibu mpaka atakapofahamu falsafa za timu hiyo.
"Huyu sio mshambuliaji ambaye anaweza kuja na kumpa nafasi haraka, nafasi ambazo mchezaji anaweza kuja na ukaona uwezekano wa kumpa nafasi ya kucheza hata kwa dakika 20,” alisema Nabi.
Aliongeza licha ya kupoteza mechi huko Tunisia, bado anawaamini mabeki wake waliopo ambao ni Yannick Bangala, Bakari Mwamnyeto na Dickson Job.
Wakati huo huo Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema suala la kiungo wao Feisal Salum ‘Fei Toto' liko vizuri na keshokutwa atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaokuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
“Fei Toto ni mchezaji halali wa Yanga, suala la yuko kambini au hayupo, Jumapili tutakapocheza dhidi ya TP Mazembe, atakuwa sehemu ya wachezaji wote uwanjani,” alisema Kamwe na kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi katika mechi hiyo.
Kauli hiyo ya Yanga imekuja baada ya gazeti hili kuandika sintofahamu iliyokuwapo kati ya klabu hiyo na Fei Toto imemalizika na Mzanzibari huyo amesaini mkataba mpya wa miaka miwili.
Inadaiwa Fei Toto amelipwa Sh. milioni 350 ili kusaini mkataba huo na sasa atapokea mshahara wa Sh. milioni 15 kwa mwezi.










