watakaouonyesha kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Azam FC, hivyo kuwataka wapinzani wao wajiandae kukutana na pumzi ya moto.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, ambaye ndiye aliyetoa kauli hiyo, mbali na hayo amelishukuru Shirikisho la Soka nchini (TFF), kwa kuisogeza mechi yao kutoka Jumamosi mpaka Jumapili wiki hii, uwanja ukiwa ni ule ule wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Akizungumza kuelekea kwenye mechi hiyo akiwa mkoani Lindi, Ahmed, aliwatahadharisha Azam kukutana na Simba ambayo kwa sasa ipo kwenye kiwango cha juu sana cha soka si la Tanzania, bali barani Afrika.
"Ni mechi ya muhimu sana kwetu, ni ya kutupeleka fainali na kama tutacheza kama tulivyocheza dhidi ya Wydad Casablanca mpaka mashabiki wa timu hiyo wakaufanya uwanja kuwa sehemu ya kufanyia sala, Azam FC anatusumbuaje? Na itakuwa ni maajabu makubwa, unampelekea pumzi ya moto Wydad ya Morocco, halafu anakuja mtu kutoka Chamazi kukusumbua kweli, yatakuwa ni mambo ya kushangaza dunia," alisema Ahmed.
Alisema kwenye mechi hiyo wanataka waihakikishie dunia kuwa kile ndicho kiwango chao halisi na wala hawakubahatisha, na kama watacheza kwa asimilia 80 tu, basi dhahama kubwa itawakumba Azam FC.
"Nikisema hivyo nina maana ni lazima tulinde kiwango chetu, hivi sasa tupo kwenye kilele cha ubora kwa hiyo kila mechi ni lazima tucheze kwa kiwango kile kile, si leo umecheza asilimia 80, kesho 20, kesho kutwa 60, yaani inakuwa ni kama unabahatisha maisha hivi.
"Tunatakiwa tucheze huku kila Mwanasimba akiwa 'anainjoi'. Tunataka kuona mashabiki wetu wakiangalia mechi za timu yetu wawe kama wanaangalia tamthilia tamu ya mahaba, siyo unatazama mpira umeshikilia roho," alisema meneja habari huyo.
Awali, Simba na Azam zilikuwa zicheze mechi hiyo Jumamosi, lakini TFF iliusogeza mbele mchezo huo, huku pia ikiuahirisha mwingine wa nusu fainali kati ya Yanga na Singida Big Stars uliokuwa uchezwe Mei 7, kwenye Uwanja wa Liti, Singida, hadi utakapopangiwa tarehe nyingine, baada ya kulikubali ombi la Yanga ambayo iliiomba mechi hiyo isogezwe mbele ili kupata nafasi ya kujiandaa na mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Marumo Gallants utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Mei 10, mwaka huu.










