Mandonga ulingoni Dodoma

04May 2023
Saada Akida
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mandonga ulingoni Dodoma

BONDIA wa Ngumi za Kulipwa nchini, Karim Mandonga, anatarajia kupanda ulingoni Juni 24, mwaka huu, dhidi ya Alick Mwenda wa Malawi katika pambano litakalofanyika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

 

Mandonga anapanda ulingoni kwenye pambano hilo ikiwa ni miezi miwili tangu amchape Kenneth Lukyamuzi wa Uganda nchini Kenya katika pambano la kuwania mkanda wa Ubingwa wa PST Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza na Nipashe jana, Mandonga, alisema anatarajia kurejea ulingoni kuzichapa dhidi ya Mwenda wa Malawi katika pambano la raundi nane.

Alisema anaendelea kufanya mazoezi ya kujiandaa na pambano hilo kuhakikisha anafanya vizuri na kumpiga mpinzani wake kwa raundi ya mapema ikiwezekana kwa KO.

"Nashukuru Mungu nipo sawa natarajia kurejea ulingoni pale Dodoma, hii kwangu itakuwa ni mara ya kwanza kupigana ndani ya Jiji la Dodoma, 'Mandonga Mtu Kazi', niwaambie mashabiki wangu nakuja huko kufanya maajabu.

"Huyo Mwenda anatakiwa ajiandae kweli kwa sababu tayari nimeshaingia kambini kwa ajili ya pambano hilo, anatakiwa kujua nishapiga watu nje na kuipa sifa kubwa Tanzania, basi na yeye nitampiga na kuendelea kuipa sifa nchini yangu katika pambano langu hilo," alisema Mandonga.

Mandonga amekuwa kivutio kikubwa katika ulingo wa masumbwi huku akiwavutia watu wengi katika Ukanda wa Afrika Mashariki kuupenda mchezo huo.

Hiyo ni kutokana na mikwara ambayo amekuwa akiitoa kabla ya kupanda ulingoni jambo ambalo mashabiki wa ngumi wamekuwa upande wake awe ameshinda ama kushindwa na mara nyingi wamekuwa wakieleza wanafurahi zaidi akipigwa maana ndiyo huongeza vibweka vyake.