Simba, Yanga zakimbiana FA

16Mar 2023
Saada Akida
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba, Yanga zakimbiana FA
  • ***Kila upande watamba kufanya vizuri katika michuano hiyo ili...

MABINGWA watetezi wa mashindano ya Kombe la FA, Yanga itakutana na Geita Gold FC ya Geita katika mechi ya hatua ya robo fainali ya michuano hiyo wakati Wekundu wa Msimbazi, Simba wao watawakaribisha Ihefu SC kutoka Mbarali, Mbeya imefahamika.

 

Mechi hizo za robo fainali zimepangwa kuchezwa kati ya Aprili Mosi na 6, mwaka huu.

Yanga itawakaribisha kwa mara nyingine Geita Gold FC kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam wakati Simba itaendelea kutumia dimba la Uhuru.

Mechi nyingine za robo fainali zitakuwa ni kati ya Azam FC dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex na Singida Big Stars watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Liti kuwaalika Mbeya City.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, alisema mechi ya hatua ya nusu fainali ya kwanza itapigwa kati ya mshindi wa mchezo kati ya Simba na Ihefu dhidi ya mshindi wa mechi ya Mtibwa na Azam wakati nusu fainali ya pili itamkutanisha mshindi wa mchezo kati ya Yanga na Geita Gold FC dhidi ya Singida Big Stars na Mbeya City.

Kizuguto alisema tarehe za michezo hiyo zimepangwa kwa kuzingatia ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na ushiriki wa timu za hapa nyumbani katika mashindano ya kimataifa.

“Tunatarajia kutumia viwanja viwili katika hatua ya nusu fainali, mchezo wa nusu fainali ya kwanza utachezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona ulioko Mtwara na nusu fainali ya pili utachezwa CCM Liti na fainali itafanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga,” alisema Kizuguto.

"Tunawakumbua wenyeji kuendelea kuboresha viwanja, endapo kiwanja hakitakidhi mahitaji, hatutasita kupeleka mashindano sehemu nyingine," Kizuguto aliongeza.

Mkurugenzi wa Wanachama wa Simba, Hamisi Kisiwa, alisema wamepokea vizuri droo hiyo na wanawaheshimu Ihefu kwa sababu ni timu nzuri, hivyo watajiandaa vyema kuwakabili ili kuvuka hatua hiyo na kucheza nusu fainali.

“Tunaenda kucheza na Ihefu FC kwa tahadhari kubwa na tutawakomboa ndugu zetu waliopo kifungoni kwa mpinzani wetu huyo ambaye kuna wenzetu walishindwa kupata matokeo mazuri,” alisema Kisiwa.

Naye Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema Yanga itaendelea kujiimarisha ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika mbio za kutetea taji hilo.

“Geita Gold FC tulikutana nao katika ligi mara mbili na zote tumewafunga, sasa tunaenda kujiandaa vyema kuwakaribisha tena kupata kichapo na kucheza nusu fainali ya ASFC, ili kufikia malengo yetu ya kucheza nusu na fainali," alisema Saleh.

Ibrahim Mohammed, Mratibu wa Singida Big Stars, alisema kuelekea mchezo huo dhidi ya Mbeya City, wamejiandaa vyema kutumia uwanja wa nyumbani kwa kupambana na kusaka nafasi ya kucheza nusu fainali.

Ofisa Habari wa Azam FC, Hashim Ibwe, alisema malengo yao makubwa ni kufanya vizuri katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ili wasonge mbele na kukaribia malengo yao.

“Mtibwa Sugar inatakiwa kujipanga vizuri kwa sababu tunamhitaji mshindi wa kwanza wa robo fainali kati ya Simba dhidi ya Ihefu FC, kwa upande wetu tunamhitaji sana Simba,” alisema Ibwe.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Ramadhani Misiru, amewapongeza TFF na Azam Media kwa kuendelea kuboresha droo ya michuano hiyo ambayo hufanyika kwa uwazi na weledi.

“Mkoani (Dar es Salaam), kwetu tuna mechi tatu, tunakaribisha wageni wetu, tunaamini mechi zitakuwa nzuri na timu zetu zina uhakika wa kufanya vizuri,” alisema Misiru.

Bingwa wa michuano hiyo hupata tiketi ya kuiwakilisha Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo hufanyika kila mwaka.