Simba, Yanga mawindoni CAF

14Mar 2023
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, Yanga mawindoni CAF

MAPEMA tu baada ya kumaliza majukumu yao ya mechi za Ligi Kuu Bara, Simba ikiirarua Mtibwa Sugar mabao 3-0 Jumamosi iliyopita huku Yanga ikishinda 3-1 dhidi ya Geita Gold FC juzi, miamba hiyo ya soka nchini imeanza maandalizi kuelekea mechi zao za kimataifa mwishoni mwa wiki.

Simba itaikaribisha Horoya AC ya Guinea katika mechi ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi wiki hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kesho yake, Jumapili Yanga kuvaana na US Monastir ya Tunisia uwanjani hapo kwenye mchezo wa Kundi D wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Kuelekea mechi hiyo, Klabu ya Simba imesema haiko tayari kuishia hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa inayoendelea, badala yake inataka kutinga robo fainali na kuendelea kama mambo yataenda kama yalivyopangwa.

Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema kwa sasa timu ya Simba hadhi yake si ya kuishia hatua ya makundi, hivyo kwa namna yoyote ile wamejiandaa kuhakikisha wanatinga hatua ya robo fainali.

"Horoya ni timu nzuri, lakini kama tukiungana, wachezaji, viongozi na mashabiki wale tunawamudu, hawatokuwa na maajabu ya kutushinda, hasa nyumbani kwetu, kwao walitufunga bao moja, lakini shughuli waliiona, sasa wanakuja kwetu na hii ni mechi ya kuamua nani aende na nani abaki. Simba hatuko tayari kubaki makundi. Hatuko tayari kwa namna yoyote ile kuishia hatua ya makundi, kwa miaka ya karibuni sisi siyo timu ya kuishia makundi kwa hali yoyote ile, hadhi yetu ni robo fainali kwanza, baada ya hapo sasa chochote kinaweza kutokea, lakini hatutafika huko na maneno ila kwa vitendo, kila mmoja atimize wajibu wake," alisema Ahmed.

Alisema wanajivunia klabu yao kuwa na wanachama na mashabiki wengi ambao wanajitolea kwa hali na mali, ikiwamo kujazana uwanja kwenda kuwashangilia tofauti na baadhi ya klabu kama Mamelodi Sundowns au Azam zinazohaha kuvutia watu waende viwanjani.

"Leo hii unatazama timu kama Mamelodi Sundowns mechi yao kubwa, lakini kiingilio ni bure, unajua kwa nini? Ni kwa sababu hawana mashabiki, wanafanya kuwavutia watu waende mpirani kwenye mechi zao. Msimu huu tangu ligi imeanza mechi za Azam pale Chamazi ni bure, ni kwa sababu hawana na wao wanafanya kuvutia watu waende uwanjani, lakini Simba tunao mashabiki, tena wenye uwezo wa kuamua kwenda uwanjani na si lazima kuwafanyia bure, wana uwezo wa kwenda uwanjani kwa kiingilio kwa hiyo wanatakiwa wajitokeze kwa wingi Jumamosi."

Kwa upande wa Yanga, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Nesreddine Nabi, naye ameanza mapema maandalizi ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir, ambapo amesema anahitaji washambuliaji kusaka matokeo mapema kwa kuongeza nguvu ya kujiamini na kucheza kwa utulivu hasa dakika za mwanzo za mchezo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Nabi aliwasifia wachezaji wake kucheza vizuri dhidi ya Geita Gold FC, lakini ameona madhaifu katika mchezo huo ikiwa ni pamoja na safu ya ushambuliaji kutotafuta matokeo ya mapema.

“Tunakutana na timu imara, na lazima tunahitaji matokeo, tunapaswa kufanya kazi kubwa kwenye kutumia nafasi za mwanzo zitakazotufanya tuwe imara na kupata matokeo mazuri, hii si mechi ya ligi bali tunahitaji ushindi," alisema Nabi.

Alisema US Monastir wako imara, na wana wachezaji wazuri ingawa hata wa Yanga ni wazuri lakini suala la kutumia nafasi wanazotengeneza bado ni tatizo kwao.

Nabi alisema wanarejea katika uwanja wa mazoezi kufanyia kazi madhaifu yaliyojitokeza mechi ya Geita Gold FC ambayo walipata ushindi mzuri, ili kuweza kushinda dhidi ya US Monastir.

Endapo Simba na Yanga zitashinda mechi zao hizo, Jumamosi na Jumapili zitakuwa zimefuzu hatua ya robo fainali na hiyo kuwa mara ya kwanza katika historia ya soka la Tanzania kwa miamba hiyo kwa msimu mmoja yote kutinga hatua ya robo fainali.

Imeandikwa na Adam Fungamwango na Saada Akida