- mechi ikichezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Ni ushindi unaowaweka sehemu nzuri ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2023/24, ikiendelea kushikilia usukani wa Ligi ya Championship, ikiwa na pointi 53, ikicheza mechi 21, kushinda 17, sare mbili na kupoteza mbili, ikibakisha mechi tisa tu kumaliza mechi zake msimu huu.
Mabao ya washindi yalifungwa na Edward Songo dakika ya 10, Elia Ashley dakika 72 na Mohamed Bakari dakika ya 83.
JKT Tanzania inaongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi 11, juu ya Kitayosce ambayo inashika nafasi ya pili kwa pointi 42 mpaka sasa.
Matokeo ya mechi zingine, Biashara United ililazimishwa suluhu kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Karume, Musoma mkoani Mara dhidi ya Mbuni FC.
Matokeo hayo yanaifanya Biashara kuwa kwenye nafasi ya tisa kwa pointi 26, Mbuni ikiwa ya nane ikifikisha pointi 30.
Kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa, KenGold iliichapa Mashujaa mabao 2-1, ikiifanya kufikisha pointi 33 kwenye nafasi ya sita, Mashujaa wakisalia kwenye nafasi ya tano na pointi zao 35.
Kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, wenyeji Ndanda walikiona cha moto kwa kutandikwa mabao 3-1 dhidi ya Fountaine Gate.
Hali si nzuri kwa Ndanda, kwani ina pointi 13 tu ikiwa nafasi ya 15 na kama itaendelea na mwenendo huo inaweza kushuka daraja kwenda Ligi Daraja la Pili.
Copco nayo iliidungua African Sports bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.










