Simba yaifanyia mauaji Ihefu

08Apr 2023
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Simba yaifanyia mauaji Ihefu

MABAO matatu 'hat-trick' yaliyofungwa na Mkongomani, Jean Baleke, Saido Ntibazonkiza na Pape Sakho yaliipa Simba ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Ihefu na kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la FA katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam jana usiku.

Kwa matokeo hayo sasa ni rasmi Simba na Azam zitakumbana katika hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo. 

Mpaka kufikia hapo, tayari Simba imecheza mechi nne ikifunga mabao 18 na kufungwa bao moja, huku Ihefu ambayo haikuruhusu mabao lolote katika mechi tatu za nyumbani ilizocheza hadi kutinga hatua ya robo fainali, ikiruhusu magoli matano kwenye mechi moja. 

Simba ilianza mechi kwa kasi na haikushangaza dakika ya pili tu kufanikiwa kuandika bao la kwanza lililofungwa na Beleke kufuatia mkwaju wa faulo uliopigwa na Clatous Chama uliotua kwenye kichwa cha mfungaji licha ya juhudi za kipa, Shaaban Kado kujaribu kuokoa kushindikana. 

Kwanza aliudaka, halafu ukamponyoka na kuvuka mstari, licha ya juhudi zake za kuudaka tena kwa mara ya pili lakini waamuzi wa mechi hiyo wakiongozwa na Jonesia Rukyaa wakamwambia aupeleke mpira kati. 

Dakika ya 15, Beleke alifunga bao la pili, alikuwa ni Kibu tena aliyemzidi nguvu kiungo, Peter Mwalyanzi katikati ya uwanja, akaukokota mpira kwa umbali mrefu na kuupiga upande wake wa kushoto alipokuwa Baleke, ambaye alipiga hatua kadhaa kabla ya kuachia kombora kali la mguu wa kushoto na kutinga wavuni. 

Beleke alikamilisha 'hat-trick' yake dakika ya 33 akifunga bao rahisi kwa mpira wa kumalizia akipata krosi pasi kutoka kwa Israel Mwenda. 

Dakika sita baadaye Mrundi Ntibazonkiza aliukwamisha mpira wavuni akiandika bao la nne ambalo lilitokana na Kado na beki wake, Yahaya Mbegu kupasiana karibuni na lango, lakini beki huyo alianguka na Mwenda akaupitia mpira kabla ya kummegea mfungaji. 

Kipindi cha pili Ihefu ambayo haikupiga shuti lolote langoni mwa Simba kipindi cha kwanza ilibadilika na kuanza kusukuma mashambulizi ikipata faulo mbili za haraka haraka na moja ikazaa bao bao dakika ya 61 kupitia kwa kichwa kilichopigwa na Rafael Daudi. 

Wakati kila mmoja akiamini matokeo hayo yatabaki kama yalivyo, Sakho aliyeingia kipindi cha pili alipachika bao la tano, Masalanga aliyeingia kipindi cha pili badala ya Kado naye akionja uchungu ya kufungwa. 

Wachezaji wa Simba waliokoa mpira kwenye lango lao na kupigiana pasi fupi fupi, kabla ya kumpasia Chama ambaye atimua mbio kwenda mbele na kumpa pasi ya upendo Msenegal huyo ambaye hakufanya ajili, akauweka ndani ya kimia. 

Wakati huo huo, habari kutoka Simba zinasema siku za kipa chaguo la pili la timu hiyo, Beno Kakolanya, kuishi katika klabu hiyo zinahesabika baada ya kubainika ameshasaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Singida Big Stars katika msimu ujao. 

Kutokana na sababu hiyo, Kakolanya ambaye alitakiwa kuanza katika mechi ya  Kombe la FA dhidi ya Ihefu iliyochezwa jana usiku, aliondolewa na nafasi hiyo ikarudishwa kwa Aishi Manula, ambaye alikuwa amepewa ruhusa kurudi nyumbani.