Simba Queens yafunguka ubingwa 2022/23 uko wazi

08Apr 2023
Saada Akida
Nipashe
Simba Queens yafunguka ubingwa 2022/23 uko wazi

KOCHA Mkuu wa Simba Queens, Charles Lukula (pichani), amesema 'ngoma ni nzito' katika vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania kwa msimu huu ambao umeshaingia katika mzunguko wa lala salama.

Lukula aliliambia gazeti hili kikosi chake kitaendelea kupambana ili kushinda mechi zao zote tano zilisalia na hatimaye kutetea ubingwa wanaoushikilia. 

Kocha huyo alisema wanahitaji kuendelea kujiimarisha kwa sababu timu tatu zilizoko katika nafasi ya juu kwenye msimamo wa ligi hiyo zina nafasi ya kushinda taji hilo. 

"Mpaka sasa hakuna mwenye uhakika wa kutwaa ubingwa, ligi ina ushindani mkubwa, na niseme lolote linaweza kutokea," alisema Lukula. 

Aliongeza ushindani uliopo unawasaidia kuongeza bidii kwa sababu bado wanataka kupata tiketi ya kushiriki tena katika mashindano ya kimataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), na baadaye Afrika. 

"Tunaamini nafasi ya kutetea ubingwa wa Tanzania tunayo, tunataka pia tukatete ubingwa wa CECAFA, ni lazima tuendelee kuonyesha ubora wetu katika kila mechi ili tufikie malengo, kila mchezaji anafahamu hilo," aliongeza kocha huyo raia wa Uganda. 

Katika kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi la Simba, mabosi wamemwajiri, Fatuma Omary, kuwa kocha mpya wa magolikipa akitokea KMC FC ya Ligi Kuu Tanzania Bara. 

JKT Queens yenye pointi 31 ndio vinara wa ligi hiyo wakifuatiwa na Simba Queens yenye pointi 30 huku Fountain Gate Princess ikifuatia ikiwa na alama 29.