Hivyo ili kutimiza azma hiyo wameanzisha kaulimbiu ambayo itatumiwa kuelekea kwenye mechi yao ya robo fainali, isemayo 'Tunavunja mwiko'.
Jumamosi iliyopita, Simba ilifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuiangamiza Horoya ya Guinea mabao 7-0, na kufikisha pointi tisa kwenye Kundi C, ikiwa ni mara ya tatu kwenye Ligi ya Mabingwa na mara moja kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Hata hivyo, Simba imefuzu hatua hiyo ikiwa bado ina mechi moja mkononi dhidi ya Raja Casablaca ya Morocco, ambayo ni kinara wa Kundi hilo la F.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema baada ya safari zote za timu yao kuishia hatua hiyo, safari hii hawatokubali na wanaelekea kucheza mechi ya robo fainali wakiwa na kaulimbiu ya 'Tunavunja Mwiko.'
"Safari hii kaulimbiu yetu kwenye robo fainali ni 'Tunavunja Mwiko'. Maana yake ni tunavunja mwiko wa kuishia robo fainali, tumeshafuzu sana robo fainali, tumeshacheza sana, hii ni ya nne, Ligi ya Mabingwa tatu na Shirikisho moja. Tumekuwa tukiishia hapa hapa, safari hii tunavunja mwiko wa kuishia hapa na kwenda hatua inayofuata zaidi.
"Ukitazama timu ambazo zinaonekana tunakwenda kucheza nazo ni Mamelodi Sundowns, Wydad Casablanca, JS Kabylie, Al Hilal, Esperance au CR Belouizdad, mimi niseme mpinzani yeyote yule kati yao, sisi tuko tayari kucheza nao, wakati tunakwenda kucheza ligi hii, tulijua tunakwenda kucheza na wakubwa wenzetu na wakubwa wengine waliotuzidi," alisema Ahmed.
Akizungumzia ushindi mkubwa dhidi ya Horoya, alisema Simba imeweka historia kubwa kwenye soka la nchi hii kwa sababu mara nyingi timu za Tanzania ndizo ambazo zimekuwa zikifunga mabao mengi na si kushinda.
"Tumezoea kuona mabao mengi zikifungwa timu za Tanzania, lakini safari hii ni kinyume chake, mabao mengi imefunga timu ya Tanzania kwa hiyo ni historia kubwa tumeiweka, pia ni historia kubwa barani Afrika kwenda kupata ushindi wa mabao saba na iliyofungwa si mtu wa kawaida, ni Horoya ambaye ni mbabe kwenye michuano hii ya Ligi ya Mabingwa, lakini Jumamosi iliyopita alijichanganya akala pumzi ya moto.
"Mnyama anaingia kwenye robo fainali kwa kishindo kweli kweli, na mechi zote zilizochezwa wiki hii, ni Simba pekee ndiyo iliyopata ushindi mkubwa wa mabao 7-0, hivyo unaona ni kazi kubwa na nzuri iliyofanywa kuweza kuandika ushindi huo. CAF imetikisika, Afrika imeogopa na Guinea wametetemeka," alisema.
Pamoja na kufuzu, Ahmed alisema watakwenda kucheza mechi ya mwisho ya makundi wakiwa na ari ile ile na hawatoidharau kwa kuwa wameshafuzu.
"Tutaenda Morocco kucheza kwa umakini ule ule kwa sababu mpira wa miguu usipouheshimu mchezo uwe wa kirafiki, uwe na umuhimu au hauna, jukumu lako ni kucheza kwa heshima ile ile kwa sababu ukiuchukulia poa na ukifungwa mabao mengi, unabaki na rekodi mbaya ndani ya timu yako, kwa hiyo tutakwenda kucheza mechi yetu na Raja Casablaca Machi 31, mwaka huu, tukiwa na ubora ule ule," alisema meneja habari huyo.










