"Mmoja acheni waje".
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Wanawake ambao Yanga Princess ni mwenyeji, waamuzi watakaoamua mechi hiyo ni Jonesia Rukyaa atakuwa kati akisaidiwa na Janet Balama na Fatma Mambo.
Katika mchezo huo Simba Queens inahitaji ushindi ili kuendelea kung'ang'ania kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo huku Yanga Princess nao wakihitaji matokeo mazuri ili kuweza kupanda juu ya msimamo wa ligi hiyo.
Simba Queens wapo kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 26 sawa na Fountain Gate iliyopo nafasi ya pili kutokana na kuzidiwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, wakati JKT Queens akishika nafasi ya tatu kwa alama zake 25 na Yanga Princess ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 21.
Timu hizo zinashuka dimbani zikiwa na kumbukumbu ya mechi ya mzunguko wa kwanza kutoka sare ya bao 1-1, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa Simba, Charles Lukula, akizungumza na Nipashe jana, amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya kutafuta pointi tatu dhidi ya Yanga Princess leo.
Alisema hana majeruhi hata mmoja na mechi itakuwa ya ushindani mkubwa kwa sababu kila mmoja wao anahitaji pointi ili kufikia malengo yao.
“Mechi ya kwanza tulicheza tukiwa nafasi ya nne, kesho (leo)tunacheza tukiwa nafasi ya kwanza, hatuhitaji kupoteza hata mechi moja, hii ni 'dabi', kama tunahitaji kuchukua ubingwa lazima tujitume kupambana kwa ajili ya kutafuta matokeo mazuri,” alisema na kuongeza:
"Ligi imekuwa ngumu sana, kila timu inahitaji matokeo katika michezo yao, tunajua Yanga Princess wanahitaji alama katika mchezo wetu na sisi tunapambana kusaka ushindi ili kufikia malengo ya kila mechi kutafuta alama tatu bila ya kujali tunacheza na timu gani,” alisema Lukula.
Aliongeza kuwa mechi ya awali hawakuifahamu vema Yanga Princess, lakini amewaona madhaifu na ubora wao hivyo, anajua ataingia na mbinu gani ili kutafuta ushindi katika mchezo wa leo.
Kocha Msaidizi wa Yanga Princess, Fred Mbuna, alisema wako salama na wamefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya mchezo wao wa leo.
Alisema wamefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika michezo miwili iliyopita ambayo walipata sare dhidi ya Mkwawa Queens na sasa wanahitaji matokeo mazuri katika mchezo huo wa dabi.
“Nimetengeneza timu yangu kwa ajili ya kucheza mchezo wa dabi kwa kufanyia kazi madhaifu ya kikosi chetu pamoja na kufahamu ubora wa wapinzani wetu, ninaimani tutaonyesha mpira mzuri,” alisema Mbuna.










