Simba Muheza watoa misaada

19Sep 2021
Steven William
MUHEZA
Nipashe Jumapili
Simba Muheza watoa misaada

KATIKA kusheherekea Simba Day mashabiki na viongozi wa timu hiyo katika Tawi la Majengo Shimoni lililoko kwenye Wilaya ya Muheza jijini Tanga wametoa misaada mbalimbali kwa watoto wenye mahitaji maalum wa Shule ya Msingi Mbaramo.

Mashabiki wa tawi hilo walifika katika shule hiyo kwa maandamano kutoka kwenye tawi lao na kupitia Kituo Kikuu cha mabasi Muheza, mtaa wa Amtico, Majani Mapana, Mbaramo mahakamani hadi kuingia kwenye eneo la shule na kukabidhi misaada hiyo huku wakisindikizwa na burudani ya muziki.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu wa Tawi la Majengo Shimoni, Fraternus Siliro, alisema viongozi na mashabiki wa tawi lao waliungana na wenzao wa Kicheba kutoa misaada hiyo kama sehemu ya kuwa karibu na jamii.

Siliro alisema mashabiki hao waliguswa na mazingira wanaoishi watoto hao na kuamua kuchanga fedha ambazo zilisaidia kununua vifaa ambavyo watoto hao walikuwa wanavihitaji.

Alitaja baadhi ya vitu walivyotoa ni vyakula, sabuni, maji na mifuko ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa mabweni ya kulala wanafunzi hao ambao ujenzi wake unaendelea.

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Halima Bulembo alisema kitendo walichokifanya mashabiki hao kinapaswa kuigwa na mashabiki wa timu nyingine.