Yanga yamaliza 'hesabu' Nigeria

19Sep 2021
WAANDISHI WETU
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Yanga yamaliza 'hesabu' Nigeria
  • ***Wakati Simba Day ya kibabe leo huku Azam FC ikitakata CAF...

KIKOSI cha Yanga kinatarajia kuwakabili Rivers United katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Adokiye Amiesimaka jijini Port Harcourt, Nigeria kikiwa na ari na 'mzuka' wa hali ya juu.

Yanga itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa bao 1-0 na wenyeji wao, walipokutana katika mechi ya kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Msemaji wa Yanga, Haji Manara aliliambia gazeti hili walifika salama nchini Nigeria jana alfajiri na jioni walitarajia kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo wa marudiano.

Manara alisema mechi zozote za mashindano ya Ligi ya Mabingwa zinazochezwa ugenini lazima ziwe ngumu na tunafahamu ugumu tutakaokutana nao tangu tutakapotua kwenye ardhi yao mpaka tutakapoondoka.

Alisema wachezaji, viongozi na mashabiki wote wa klabu hiyo walioko Nigeria wako tayari kwa ajili ya mechi hiyo na wanaamini ushindi utapatikana na hatimaye kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

"Kesho (leo), kwenye Uwanja wa Adokiye, majira ya saa 10 alasiri, mabingwa wa kihistoria watafanya mazoezi ya mwisho kabla ya mechi ya Jumapili, tuko tayari kwa ajili ya mechi hiyo, wote tulioko hapa tuko tayari... nia yetu ni kwenda kuipigania klabu yetu, kwenda kuipigania nchi yetu," alisema Manara.

Naye Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Benson Bana, aliwataka wachezaji wa Yanga wakapambane na kuhakikisha wanapata ushindi mnono katika mchezo huo.

"Nigeria ni salama, ubalozi ulijipanga, tunawaaomba mkapambane, msiwaangushe Watanzania," alisema balozi huyo.

 

...LEO NI SIMBA DAY

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, wanaikaribisha TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), katika mechi ya kirafiki ya Tamasha la Simba "Simba Day' itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini.

Tamasha hilo ni maalum kwa ajili ya kutambulisha wachezaji wa Simba watakaokitumikia kikosi chao katika msimu mpya wa 2021/22.

Simba kwa mara ya kwanza inaingia katika mchezo huo huku benchi la ufundi likiwa na makocha watatu Didier Gomes ambaye atasaidiwa na Thierry Hitimana na Seleman Matola.

Akizungumza jijini jana, Gomes, alisema anafuraha kubwa kukutana na Mazembe ambao ni wapinzani sahihi kwao katika maandalizi ya msimu mpya.

"Nataka kuwaonyesha mashabiki wetu kile tulichokuwa nacho, nawajua Mazembe tulikutana katika mashindano ya Simba Super Cup, walitupa changamoto nzuri, nina furaha kukutana nao tena," alisema Gomes.

Nahodha wa Simba, John Bocco alisema wamekuwa na maandalizi mazuri kuelekea msimu mpya na kukutana na TP Mazembe kwao ni kipimo bora.

Wakati huo huo Azam FC imesonga mbele katika mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 4-1 dhidi ya Horseed kutoka Somalia.