Straika huyo ambaye alipachika mabao 17 akiwa amesajiliwa kipindi cha dirisha dogo la usajili, amejiunga na klabu hiyo baada ya kumaliza mkataba wake na Simba Queens, huku akiwa amesaini mkataba wa miezi sita na klabu yake hiyo mpya.
Taarifa iliyotolewa jana na klabu hiyo imeeleza kuwa hawatokuwa na mchezaji huyo kuelekea msimu ujao wa mashindano yanayowakabili.
“Mshambuliaji kinara, Jentrix Shikangwa, hatutakuwa naye msimu ujao baada ya mkataba wake kumalizika," ilieleza taarifa hiyo ya Simba.
Habari kutoka kwa baadhi ya vyombo vya habari nchini Kenya, zimeeleza kuwa straika huyo anayeichezea Timu ya Taifa ya Kenya kwa Wanawake 'The Harambee Starlets', baada ya kumaliza mkataba wake, alikuwa anawindwa na klabu mbalimbali zikiwamo Mamelodi Sundowns na Yanga Princess, lakini mwisho wa siku alikubaliana na dili la klabu hiyo ya Ligi Kuu nchini China ambalo lilikuwa nono zaidi.
Straika huyo mwenye nguvu na mashuti makali, aliwaaga na kuwashukuru mashabiki wa Simba Queens kwenye mtandao wake wa kijamii wa Instagram.
"Nashukuru Simba Queens na mashabiki wote kwa upendo wenu na sapoti yenu kwangu, ngoja tujaribu tena sehemu nyingine," alisema mchezaji huyo ambaye pamoja na kwamba hakuipa timu hiyo ubingwa, lakini aliiwezesha kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu uliomalizika.
Shikangwa ndiye alionekana kuchukua kijiti cha straika Mtanzania Opa Clement kwenye ufungaji ndani ya kikosi hicho ambaye naye aliondoka Machi mwaka huu kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Uturuki kwenye Klabu ya Besiktas.










