Katika mahojiano maalum na gazeti hili kwenye viunga vya Bunge mjini hapa mwishoni mwa wiki, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Michezo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Alex Mkenyenge, alisema mfumo huo mpya utaanza kutumika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Alisema kuwa mfuko huo pia utakuwa wa kielektroniki na utasimamiwa na moja ya kampuni tatu zilizojitokeza kuwania tenda hiyo.
Hata hivyo, alipoulizwa mmoja vigogo wa juu wa Benki ya CRDB, ambaye hakutaka jina lake kuandikwe kwenye gazeti kuhusiana na uamuzi huo wa serikali, alisema hana taarifa na uamuzi huo, ila anachofahamu ni mfumo huo umeshimamishwa kwa muda tu ili kushughulikia changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake.
“Nachofahamu mkataba haujavunjwa ila mfumo umesitishwa kwa muda ili kushughulia matatizo kadhaa yaliyojitokeza nyuma. Lakini pia hata kama kweli mkataba umevunjwa, kuna mambo ya kisheria lazima yaangaliwe,” alisema kigogo huyo.
Mkenyenge alisema: "Baada ya kusitishwa kwa matumizi ya tiketi za elekroniki za CRDB, Wizara iliwaagiza Beijing Construction (kampuni iliyojenga Uwanja wa Taifa) kusaka kampuni ambayo itasimamika mfumo mwingine mpya wa ukusanyaji mapato kwenye Uwanja wa Taifa.
Kampuni tatu zilijitokeza kuomba tenda hiyo; Max Malipo, Selcom na I-Pay. Tayari mmoja wao ameshinda tenda, lakini siwezi kumtaja kwa kuwa mimi si msemaji wa Beijing Construction).
Tayari usimikaji wa mfumo huo umekamilika kwenye Uwanja wa Taifa, kilichobaki ni Beijing Construction kupitia kwa Mshauri Mwelekezi wa Wizara, watukabidhi mradi huo. Tuna uhakika, utaanza kufanya kazi kuanzia msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara."
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema jana kuwa mkataba huo upo kisheria na ulisainiwa na viongozi wa juu wa TFF.
“Viongozi wa juu wa TFF ndiyo waliongia mkataba na CRDB, kama kuna ufafanuzi wahusika ni rais na katibu mkuu,” alisema Wambura. Hata hivyo, juhudi za kumtafuta Jamal Malinzi na katibu wake zilishindikana kutokana na simu zao kuita bila kupokelewa.
Kusimikwa kwa mfumo huo mpya kuna maana, serikali imeachana rasmi na mfumo wa tiketi za kielektroniki uliokuwa unasimamiwa na CRDB msimu uliopita wa Ligi Kuu.
Kabla ya kutoa uamuzi huo, serikali ilitangaza Machi 4, mwaka jana kusitisha matumizi ya tiketi za mfumo wa CRDB kwenye Uwanja wa Taifa kwa maelezo kuwa mfumo huo ulikumbwa na changamoto katika utekelezaji wake.
CRDB ilishinda tenda iliyotangazwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mwaka 2013 ya kusimika mfumo wa tiketi za kieletroniki kwenye viwanja vya soka nchini.
Licha ya kutumia Sh. bilioni tatu kusimika mfumo huo, benki hiyo iliendesha kwa muda mfupi mfumo wa tiketi za kielekroniki kwenye baadhi ya viwanja vya soka, kisha ukasitishwa na serikali kwenye Uwanja wa Taifa na kusababisha kusitishwa pia kwenye viwanja vingine.










