Serikali kutia mkono gofu

28Mar 2023
Shufaa Lyimo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serikali kutia mkono gofu

WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, imesema itatumia nguvu nyingi kuwekeza kwenye michezo yote nchini ukiwamo wa gofu ili kuondoa dhana kuwa mchezo unaungwa mkono zaidi nchini ni mpira wa miguu.

 

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam juzi usiku na Naibu Waziri wa  Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma 'Mwana FA', wakati akifunga shindano la NBC Lugalo Open 2023.

"Wizara imejipanga kuinua michezo yote hapa nchini kwa lengo la kuitangaza nchi yetu kupitia michezo, ili kuunga mkono juhudi za rais wetu kwa vitendo," alisema Mwinjuma.

Aidha, waziri huyo aliipongeza Klabu ya Gofu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Lugalo (TPDF), kutokana na juhudi wanayoifanya kuibua vipaji kwa upande wa vijana, pamoja na kuruhusu raia kushiriki mashindano katika viwanja vyao.

Pia aliishukuru Benki ya Taifa ya Biashara NBC kutokana na kazi kubwa wanayoifanya ya kudhamini michezo mbalimbali ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara na kuzitaka taasisi nyingine ziige mfano huo.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Klabu ya Lugalo, Brigedia Jenerali  Mstaafu, Michael Luwongo, alisema klabu hiyo ni miongoni mwa klabu inayofanya vema katika mchezo huo.

Alisema shindano hilo lililomalizika  lilishirikisha wachezaji 150 kutoka klabu zote za gofu Tanzania na kuwapongeza washindi wote.

Katika shindano hilo mshindi wa jumla alikuwa ni Ally Isanzu kutoka   Klabu ya TPC Moshi mkoani Kilimanjaro, ambaye amepata makombe mawili pamoja na zawadi ya friji, huku upande wa wanawake akiwa ni Hawa Wanyeche, aliyezawadiwa jiko la umeme pamoja na kombe.