Azam, Gor Mahia basi tena, kukiwasha na KMC FC leo

28Mar 2023
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Azam, Gor Mahia basi tena, kukiwasha na KMC FC leo

KLABU ya Azam FC imetangaza rasmi kuwa haikwenda nchini Kenya kucheza mechi yake ya kirafiki dhidi ya Gor Mahia kama ilivyopangwa kutokana na hali ya kisiasa nchini humo kutokuwa shwari.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Thabit Zacharia maarufu 'Zaka Zakazi', amesema awali ilipangwa mechi hiyo ingechezwa jana kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi nchini Kenya, lakini imeshindikana kutokana na sababu za hali ya kisiasa inayoendelea nchini humo kati ya serikali na wafuasi wa aliyekuwa mgombea wa kiti cha Urais, Raila Odinga.

Kutokana na hali hiyo, timu hiyo itacheza mechi yake ya kirafiki leo Jumatatu saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, dhidi ya KMC ya Kinondoni.

"Tutacheza na KMC leo, awali tulipanga kucheza na Gor Mahia, mechi ilikuwa ifanyike Jumapili Uwanja wa Nyayo, Nairobi nchini Kenya, lakini hali ya kisiasa nchini humo kwa sasa si nzuri ikabidi tutafute timu nyingine na kwa muda mfupi uliopatikana timu yenyewe ilikuwa ni hii KMC, kwanza tumeshamalizana nao mzunguko wa pili, timu zingine ni kama tumezishtukiza sana hazikuwa na muda.

"Lakini baadhi zinatuogopa zinaona tukikutana nao saa hizi  tutawazoea halafu kwenye mechi za mzunguko wa pili itakuwa matatizo, lakini kwa KMC wenyewe nao wanauhitaji kwa sababu wapo kwenye kipindi kigumu katika msimamo wa Ligi Kuu, hivyo mechi hiyo ni muhimu kwao," alisema.

Alisema baada ya mechi dhidi ya Gor Mahia kugonga mwamba kuchezewa nchini Kenya, walifikiri kuileta Tanzania, lakini muda ukakwamisha kwani ukawa mdogo kwa kila timu kuendelea na programu zake.

"Tulifikiria kama kuileta Gor Mahia kucheza nchini, lakini muda umekuwa mfupi sana, badala yake tuna mechi hii kwa sababu wachezaji wakikaa muda mrefu utimamu wa mwili unapungua, hivyo ni lazima utengeneze mechi hapo katikati ili kulinda ule utimamu wao," alisema.

Azam itacheza mechi hiyo ikiwa ni maandalizi ya mchezo wao wa robo fainali wa Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) maarufu Kombe la FA dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaopigwa Uwanja wao wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.