Kipigo hicho kimeifanya kuendelea kukamata mkia ikiwa na pointi 20 kutokana na mechi 27 ilizocheza mpaka sasa, ikisalia na mechi tatu tu za kumaliza msimu.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makata, amesema watajitahidi kila njia kupata pointi tisa zilizobaki kwenye mechi tatu ili waangalie wataangukia wapi, huku wao pia wakiwa hawana ukakika na wapo tayari kwa chochote kitakachotokea.
"Tumejitahidi sana kadri ya uwezo wetu, haya yanayotokea ni kwa sababu mwanzo haukuwa mzuri, tungekuwa na mwanzo mzuri tusingefika hapa, kwenye mechi zilizosalia tutapambana na tutakubaliana na chochote kitakachotokea," alisema Makata.
Ruvu imeshinda mechi tano tu mpaka sasa kwenye Ligi Kuu msimu huu, ikiwa ni moja kati ya timu zilizoshinda mechi chache pamoja na Polisi Tanzania, huku ikipoteza mechi 17 ambazo ni nyingi kuliko timu yoyote kwenye ligi hiyo.
Pamoja na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu Ijumaa iliyopita kwenye Uwanja wa Ushirikia mjini Moshi, bado Polisi Tanzania haipo sehemu salama kwenye ligi hiyo kwani inashika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 22, mbili juu ya wanaoshika mkia Ruvu Shooting, nayo ikiwa imebakisha mechi tatu ili kujua hatma yake kama itashuka, kucheza 'play off' au kujiokoa na vyote.
Timu ya KMC, pamoja na kumchukua kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio', baada ya kumfurusha Thierry Hitimana, bado haikuwa dawa baada ya kutwangwa bao 1-0 Jumamosi iliyopita dhidi ya Dodoma Jiji katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
KMC nayo iko eneo la hatari ikiwa na pointi zake 26, nafasi ya 14, ikibakisha mechi tatu nayo kumaliza mechi zake 30 za msimu huu.










