Ndanda FC yashindwa kuifuata Capco Mwanza

25Apr 2023
Baraka Jamali
MTWARA
Nipashe
Ndanda FC yashindwa kuifuata Capco Mwanza

UONGOZI wa Klabu ya Ndanda yenye masikani yake mkoani Mtwara, imeshindwa kuisafirisha timu hiyo kuipeleka jijini Mwanza, walipopaswa kucheza mchezo namba 223 wa Ligi ya Championship dhidi ya Copco FC ambao ulipagwa kupigwa Uwanja Nyamagana leo Jumanne, kutokana na kukosa fedha.

 

Akizungumza na vyombo vya habari mkoani Mtwara jana, Mwenyekiti wa Ndanda FC, Geofrey Lukanga, alisema wameshindwa kuisafirisha timu hiyo kwenda kucheza mchezo huo kutokana na kukosa fedha ya mafuta na mahitaji mengine ya wachezaji hali iliyosababisha wachezaji kuruhusiwa kuondoka kambini.

“Tulikuwa na mchezo kesho [leo] dhidi ya Copco katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, lakini kutokana na kukosa fedha za kuisafirisha timu, tumeamua kuwaruhusu wachezaji waondoke kambini na kama tutapata fedha basi tutawataarifu ili kuwahi kucheza mchezo wa Mara [Aprili 24, mwaka huu], lakini kwa Sasa tumeshindwa kabisa kusafirisha timu,” alisema Mwenyekiti huyo.

Aliendelea kueleza: Tumewatafuta wadau akiwamo mlezi wetu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas, lakini jitihata zetu zimegonga mwamba, ili tuweze kufanikisha michezo yetu mitatu ya nje tunahitaji kuwa na milioni 25, lakini mpaka sasa tumekwama ingawa tunajua ni jambo linaloumiza, lakini kwa sasa hatuna cha kufanya zaidi ya kuifunga kambi ya timu yetu”.

Aidha, kwa upande wa Mkurugenzi wa timu hiyo na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara, Athumani Kambi, aliwaeleza waandishi wa habari kwamba alikuwa na uwezo wa kuipatia timu hiyo Sh. milioni 1.5 au mbili, lakini haikutosha kuisafirisha timu hiyo na kwamba imetumika kuwapa wachezaji hao nauli za kurejea kwao kutokana na hali hiyo mbaya.

Alisema: "Kama tukipata fedha leo tutawaomba TFF waweze kuipeleka mechi hiyo Ijumaa ili tucheze kwa sababu nia tunayo, lakini hatuna fedha kwa sasa na wadau wameonesha kutotuunga mkono kwa wakatu huu, lakini tuliwafuata ili watusaidie kuisafirisha timu, sipendezwi na uamuzi huu, lakini timu ilibaki kwangu peke yangu ila siwezi kuiendesha kwa sasa”.

Ndanda fc msimu huu ina alama 15 ikiwa nafasi ya 15 kati ya timu 16 zinazo shiriki ligi hiyo na imesaliwa na michezo minnne dhidi ya Copco ya Mwanza, Biashara ya Mara, Pan African ya Dar es salaam na dhidi ya Transit Camp itakayopigwa Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.