REFA wa kati Jonesia Refa wa kati Jonesia Kabakama Rukyaa (26) ambaye amepangwa kuchezesha mchezo kati ya Simba na Yanga Jumamosi amezionyaa klabu hizo zisithubutu wala zisifikirie kumuhonga rushwa kuelekea kwenye mchezo huo.
Jonensia ambaye aliwahi kuchezesha mechi ya kirafiki kati ya Simba na Yanga, Desemba 13, mwaka 2014 ndiye aliyekabidhiwa mechi ya Jumamosi ya Ligi.
Mpaka jana asubuhi Shirikisho la Soka nchini (TFF) tayari ilikuwa imepitisha jina ya mwamuzi huyo mwenye beji ya FIFA na kwamba inatarajia kumtangaza hadharani muda wowote.
Jonensia aliliambia Lete Raha jana saa 7 mchana, “Sina taarifa yoyote rasmi juu ya mimi kuchezesha mechi la Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga japokuwa nipo jijini Dar es Salaam kwaajili ya kozi elekezi kwa waamuzi.
“Ratiba ambayo nilikuwa nayo hapo awali ni kwamba wikiendi hii Jumamosi nilikuwa ninatakiwa kuchezesha mchezo kati ya Stand United na JKT Ruvu kwenye uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
“ Iwapo nitatakiwa kuchezesha mchezo huo basi nitachezesha kama ninavyochezesha michezo mingne ya Ligi kwa kufuata sheria na kanuni za soka. Kwanza kabisa sitavumilia timu yoyote ambaye itaonesha nia au kunishawishi kwa kunipa rushwa.
“ Rushwa ni adui wa maendeleo na pia ni moja ya mambo yanayodidimiza soka duniani kote hivyo sitasita kumfichua Yule ambaye atajaribu kunishawishi kwa kunipa rushwa. Iwe Simba au Yanga kama nitakuwa nimeteuliwa kuchezesha mchezo huo nitafanya kazi yangu vizuri,” alisema mwamuzi huyo.
Alivyochezesha mechi ya kirafiki Simba, Yanga.
Hatukuzungumza na refa huyo kuhusu masuala ya kiufundi katika mechi iliyopita ya Simba dhidi ya Yanga au mipango yake mchezo unaokuja kwa sababu kanuni za marefa wa soka haziruhusu mwamuzi kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu mechi aliyoichezesha bali anaweza kutoa ushauri kwa wachezaji juu ya kucheza soka kwa nidhamu na kwa kufuata sheria.
Jonesia ambaye Desemba mwaka 2014 aliweka historia kwa kuwa mwamuzi wa kwanza wa kike kuchezesha mchezo wa watani Simba na Yanga, alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti jazba za wachezaji lakini pia kuendana na kasi ya mchezo.
Kwenye mchezo huo mwamuzi huyo alikuwa akichezesha na mara nyingi ilipotokea mvutano alikuwa akiwachomoa wahusika pekee yake dhumuni likionekana kuwa hakutaka kushinikizwa na kundi la wachezaji ambao wangekuwa wakimzonga.










