Pazia la ligi kuu kufungwa leo

22May 2016
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Pazia la ligi kuu kufungwa leo
  • **Kazi kubwa imebaki kwa timu za Kagera Sugar, JKT Ruvu na Mgambo JKT zinazopambana kubaki ligi kuu msimu ujao.

PAZIA la ligi kuu Tanzania bara msimu wa 2015/2016 linafungwa leo kwa michezo mbalimbali huku mabingwa wa msimu huu Yanga wakiwa mkoani Ruvuma kukabiliana Majimaji ya Songea.

Wachezaji wa Yanga wakiingia uwanjani siku ambayo walitangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mwaka 2016.

Timu zote 16 zitakuwa katika viwanja tofauti kukamilisha msimu huu wa ligi huku baadhi ya timu zikiwa kwenye presha kubwa ya kukwepa kushuka daraja.

Kwa msimamo ulivyo, timu za African Sports, Mgambo JKT, Kagera Sugar, JKT Ruvu na Toto Africans ndizo ambazo zinaonekana kuwa katika vita ya kukwepa kushuka daraja. timu hizo kila moja inahitaji kushinda mchezo wake huku ikiziombea nyingine kupoteza ili kuangalia uwezekano wa kusali ligi kuu msimu ujao.

Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Mwadui katika mchezo ambao Kagera wanahitaji zaidi ushindi kujiweka katika usalama wa kubakia ligi kuu.

African Sports ambao tayari wamepeleka mguu mmoja kwenye ligi daraja la kwanza watakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar na endapo watafanikuwa kushinda mchezo huo bado itawabidi kuangalia matokeo ya Kagera na Mgambo watanaocheza na Azam FC.

Kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba watakuwa wenyeji wa JKT Ruvu katika kujaribu kuona wanamaliza ligi wakiwa nafasi ya pili lakini hilo litawezekana tu endapo watashinda mchezo huo huku wakiiombea Azam kupoteza mchezo wao.

Michezo mingine leo, Coastal Union ambayo tayari imeshuka daraja itaumana na Prisons ya Mbeya kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga wakati mchezo mwingine, Mbeya City itawakaribisha Ndanda FC kwenye uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Yanga tayari imetwaa ubingwa msimu huu na kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya klabu bingwa Afrika msimu ujao huku pia Azam FC ikiwa imejihakikishia kucheza mashindano ya kimataifa mwakani baada ya kufanikiwa kutinga fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho (FA).